TCRA YAHAMASISHA WATUMIAJI WA SIMU ZA MKONONI 'KUJANJARUKA'


Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo akizungumza wakati akimkabidhi Leseni ya Utangazaji wa Vipindi vya Redio Mkurugenzi wa Kituo cha Matangazo cha Gold Fm, Neema Mghen. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo akimkabidhi Leseni ya Utangazaji wa Vipindi vya Redio Mkurugenzi wa Kituo cha Matangazo cha Gold Fm, (88.7Mhz Sauti ya Dhahabu) Bi. Neema Mghen.
Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo akimkabidhi Kanuni za Utangazaji wa Vipindi vya Redio Mkurugenzi wa Kituo cha Matangazo cha Gold Fm, (88.7 Mhz Sauti ya Dhahabu) Bi. Neema Mghen (kulia).

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog 
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka Wamiliki wa Simu za mkononi kujanjaruka kwa kuhakiki laini zao za simu kwa kupiga *106# ili kubaini endapo namba za vitambulisho vyao vya Taifa havijatumika kusajilia laini za watu wengine huku ikiwataka kutoa taarifa pindi wanapopokea au kupigiwa simu za kitapeli kwa kunakiri ujumbe waliotumiwa au namba waliyopigiwa na kutuma kwenda namba 15040 bure.

Rai hiyo imetolewa leo Alhamis Julai 22, 2021 na Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo wakati akikabidhi Leseni ya Utangazaji wa Vipindi vya Redio kwa Kituo cha Matangazo cha Gold Fm (88.7Mhz Mhz Sauti ya Dhahabu) kilichopo Mjini Kahama Mkoani Shinyanga.

Mhandisi Mihayo ametumia fursa hiyo kuelezea juu ya Kampeni ya TCRA maarufu Janjaruka  ambayo inalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu usajili na wa namba ya simu na uhalifu.

Amesema huduma zote hizo ni bure na hakuna gharama yoyote watakayotozwa pindi watakapotumia namba hizo (*106# na 15040).

"Naomba pia Waandishi wa habari muwe mabalozi wa kutoa elimu kwa wananchi. Kila mmoja ahimize kujanjaruka kwa kuhakiki laini yake ya simu kwa kupiga *106#  au kutoa taarifa kuhusu matapeli kwa kutumia ujumbe waliotumiwa au namba iliyotumika kupiga au kutuma ujumbe kwenda 15040 bure",amesema Mhandisi Mihayo.

Aidha amesema namba 100 ya watoa huduma kwa wateja kwa Makampuni yote ya simu ndiyo namba pekee ya kupigiwa simu na wato huduma na namba hiyo hiyo itatumika kwa mteja kupiga kwa mtoa huduma


ELIMU KWA UMMA KUHUSU USAJILI NA WA NAMBA YA SÄ°MU NA UHALIFU

KWA NAMBA  106

1.    Historia ya usajili.

Usajili wa laini za simu ni zoezi la awali kabisa ambalo hufanyika mtu anaponunua laini yake ya simu ambapo mtumiaji hutakiwa kukamilisha umiliki wa laini yake kwa kuweka namba yake ya kitambulisho cha taifa ambayo itahibitisha kwa kutumia alama zake za vidole.

Usajili wa laini ni utekelezaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 na Kanuni ya Mawasiliano ya Kielektroniki ya Posta (Usaili wa laini za simu ya simu) ya 2018 ambazo zinamtaka pamoja na mambo mengine mtu yoyote anayetaka kutumia laini ya simu ahakikishe kuwa anaisajili namba hiyo kwa kutumia namba yake ya kitambulisho cha taifa.

2.    Kwanini tunahakiki?

Baada ya kukamilika kwa zoezi la usajili wa laini kulionekana mapungufu ambapo baadhi ya watu kwa kujua na wengine kwa kutojua waliwasajilia watu wengine laini zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Zoezi la uhakiki limekuja kurekebisha mapungufu hayo ambapo sasa mtumiaji amejengewa uwezo wa kuweza kuangalia ni namba ngapi zimesajiliwa kwa kutumia namba yake ya kitambulisho cha taifa na iwapo atakuta namba ambazo hazifahamu anaweza kuzitoa.

3.    Tofauti ya kusajili na kuhakiki.

Tofauti ya usajili na uhakiki ni kwamba usajili ni zoezi la awali kabisa ambalo hufanyika mtu anamponunua laini yake ya simu ambapo mtumiaji hutakiwa kukamilisha umiliki wa laini yake kwa kuweka namba yake ya kitambulisho cha taifa ambayo itathibitisha kwa kutumia alama zake za vidole.

Uhakiki ni hatua ambayo mwananchi anaifanya kujiridhisha iwapo usajili wake umekamilika na pia kuweza kutambua namba za simu ambazo zimesajiliwa kwa kutumia namba yake ya kitambulisho cha taifa.

4.    Utaratibu wa kuhakiki ukoje? (kutakuwa na foleni kama ilivyokuwa kusajili?

Utaratibu wa kuhakiki ni mwepesi sana unachotakiwa kufanya ni kubonyesha *106# alafu kufuata maelekezo. Uhakiki hufanyika kwa kutumia simu yako ya mkononi hivyo hakutakuwa na haja ya kwenda kupanga foleni kuhakiki. Wakati pekee ambao utatakiwa kwenda kwa mtoa huduma ni pale ambapo umehakiki na kukuta namba ambayo huitambui na unataka kuitoa, hapo ndipo utatakiwa kwenda kwa mtoa huduma akusaidie kuitoa.

5.    Uhakiki utasaidiaje kupunguza uhalifu?

Wahalifu wanatumia namba ambazo zimesajiliwa na watu wengine kufanyia uhalifu hivyo iwapo utahakiki namba zako na ukatoa namba zote ambazo huzifahamu lakini zimesajiliwa kwa kutumia namba ya kitambulisho chako basi utakuwa umewezesha kuzuia uhalifu maana namba hizo zitazimwa.

6.    Je ni kosa kutumia laini ambayo haijasajiliwa kwa kutumia jina na namba ya kitambulisho chako cha taifa?

Ndio, Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 na Kanuni ya Mawasiliano ya Kielektroniki ya Posta (Usaili wa laini za simu ya simu) ya 2018 zinakataza kutumia laini ambayo haijasajiliwa kwa kutumia jina na namba yako ya kitambulisho cha taifa na endapo utabainika kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wewe unayetumia na aliyetoa namba yake isajili namba ambayo haitumii yeye.

7.    Mamlaka inawataka wananchi wafanye nini?

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inawataka watumiaji wote wa huduma za simu kuhakikisha kuwa wanatumia laini ambazo zimesajiliwa kwa kutumia namba zao za vitambulisho vya taifa na wajenge utaratibu wa kuhakiki namba hizo kwa kuhakikisha kuwa anazitambua na kuridhia namba zote ambazo zimesajiliwa kwa kutumia kitambulisho chake cha taifa.

Na iwapo atakuta namba ambayo haitambui basi aende kwa mtoa huduma ili waitoe namba hiyo katika orodha ya namba ambazo anazimilikiwa kwa kutumia kitambulisho chake.

8.    Uhakiki wa simu unasaidiaje unapopotelewa na simu?

Uhakiki wa simu unakusaidia kuwa salama unapotumia huduma zako za simu. Unapopotelewa na simu hatua unazotakiwa kufuata ni kutoa taarifa polisi na kisha kwa mtoa huduma wako ili namba hiyo iweze kuzimwa na baadae uweze kupatiwa laini nyingine ya simu ambayo itakuwezesha kuendelea kutumia huduma za mawasiliano kama ilivyoawali. KWA NAMBA 15040

1.      Namba hii ni ya nini?

Hii ni namba ya huduma ambayo imetolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzanani kwa watoa huduma ili waweze kuitumia kupokea taarifa za namba ambazo zinatumika katika uhalifu.

2

2.      Namba hii iko wapi?

Namba hii iko kwa watoa huduma wote.

3.      15040 inafanyaje kazi?

Namba ya huduma ya 15040 imeunganishwa moja kwa moja na mtoa huduma hivyo mtumiaji anapotuma namba iliyofanya uhalifu kwenda kwenye namba hii mtoa huduma huipokea na kuifanyia kazi namba hiyo ambapo baadhi ya hatua ambazo huchukuliwa ni kuiripoti namba hiyo kwa mamlaka zinazohusika na kukabiliana na uhalifu na kisha kuifunga namba hiyo.

4.      Je namba hii inalipiwa?

Hapana, huduma kwenda kwenye namba hii ni bure. Hata hivyo kwa wale ambao wanatumia simu janja ambazo zinatumia mfumo wa Andriod wanapotumia huduma hii wataulizwa iwapo wako tayari kuilipia ambapo mtumiaji atatakiwa kukubali kulipia ndipo ujumbe uende japo kiuhalisia hatokatwa malipo yoyote.


Soma pia :

GOLD FM YATAMBULISHWA RASMI IKIUNGURUMA KUTOKA KAHAMA, TCRA YAKABIDHI LESENI ,KANUNI ZA UTANGAZAJI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post