Muonekano wa sehemu ya lambo kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu ambalo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amelikabidhi kwa Halmashauri ya Manispaa ya Chalinze baada ya kukarabatiwa na serikali kwa zaidi ya Shilingi Milioni 600 na kuagiza kuundwa kwa kamati ya kusimamia lambo hilo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Na. Edward Kondela
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameagiza shamba la malisho ya mifugo lililopo Vikuge Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, kujiendesha kibiashara na kusambaza mbegu za malisho kutoka nchini China ijulikanayo kama JUNCAO maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa ina sifa ya kustahimili sehemu yenye ukame ili wafugaji wapande malisho hayo.
Wakati akihitimisha ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo Naibu Waziri Ulega, amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya shamba hilo na kumuagiza Katibu Mkuu anayeshugulikia Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel kuhakikisha aina mpya ya malisho hayo inasambazwa na kusimamia vyema ili mradi huo uweze kuwa na tija kwa taifa hususan kwa wafugaji vijijini.
Mhe. Ulega amesema mbegu za malisho ya JUNCAO zisambazwe kuanzia ngazi ya mikoa wilaya hadi vijiji lengo likiwa kudhibiti mifugo na wafugaji kuhamahama kutafuta malisho.
Amefafanua kuwa hataki kuona mambo yanayoanzishwa kwa ajili ya kunufaisha wananchi yanaishia njiani kwani ni vizuri kukawa na mwendelezo wa teknolojia hiyo ya kilimo hicho kipya cha malisho ya mifugo hata kusambazwa kwa wafugaji hadi vijijini.
Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha mbegu za malisho hayo zinaenea hadi vijijini kwa wafugaji akitaja hususan mikoa yenye ukame kama Dodoma, Singida, Manyara, Shinyanga na iwapo zitasambazwa vizuri itapunguza tatizo la wafugaji na mifugo yao kuhama hama kutafuta malisho ya mifugo yao.
"Kinachosababisha wafugaji kuzunguka na kuhama hama ni kutafuta chakula cha malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao hivyo kama wafugaji watafikishiwa mahali walipo itawasaidia wafugaji kuwa na uhakika wa malisho." amesema Mhe. Ulega.
“Mbegu hizi nataka zifike kwa haraka na kwa gharama nafuu ambayo kila mfugaji ataweza kununua aweze kuhudumia mifugo yake.” amesema Mhe. Ulega
Akizungumzia changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa shamba la Vikuge Meneja wa shamba hilo Bw. Reuben Ngailo amesema kukosekana kwa vifaa na nguvu kazi katika mipango yao ya kusafisha shamba na kupanua uzalishaji.
Amesema pia eneo hilo la shamba lina visiki vingi ili kuving'oa inagharimu kiasi kikubwa cha fedha jambo ambalo husababisha kuendesha uzalishaji wa malisho katika eneo dogo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwani Kikwete akiwa ameambatana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameomba malisho yanayozalishwa shambani hapo kuwanufaisha wakazi wa Mkoa wa Pwani.
Mhe. Kikwete amesema shamba hilo lipo Mkoa wa Pwani na mkoa huo una migogoro mingi ya wakulima na wafugaji kwa ajili ya kutafuta malisho na maji, hivyo ombi lake ni mbegu hizo zisambazwe haraka kwa wafugaji wa mkoa huo.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amekabidhi lambo la kunyweshea mifugo maji la Chamakweza lililopo Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani na kuiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Chalinze kuunda kamati kwa ajili ya kusimamia lambo hilo lililokarabatiwa na serikali kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Milioni 600 kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu.
Mhe. Ulega amesema ni wakati sasa wafugaji kutumia vyema lambo hilo kwa ajili ya kuboresha mifugo yao ambayo imekuwa ikikosa maji ya kunywa na kuwataka kubadilika na kuanza kufuga kibiashara kwa kuwa na mifugo ambayo wanakuwa wanavuna kila baada ya muda kwa kuuza kwenye viwanda vya kuchakata nyama badala ya kuwa na mazoea ya kuwa na mifugo mingi ambayo haina tija kwao.
Amefafanua kuwa lengo la serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuona mfugaji ananufaika kupitia mifugo yake kwa kufanya biashara na hatimaye kuongeza pato la taifa na mfugaji mwenyewe.
Naibu Waziri Ulega tayari amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani.