Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro amesisitiza kuwa sio sifa kumiliki silaha endapo huna sifa za kuimiliki.
Amesema umiliki wa silaha una sheria zake na endapo mmiliki anazikiuka hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kifungo cha miezi 12 jela au faini ya shilingi milioni moja au vyote kwa pamoja.
Kamanda Muliro ametoa kauli hiyo kufuatia matukio la mauaji yaliyotokea hivi karibuni katika maeneo ya Sinza Mori na Mbezi Makabe mkoani Dar es Salaam, ambapo pia amewataka Viongozi wa Serikali za mitaa na wamiliki wa maeneo ya starehe kushirikiana na jeshi la polisi kuwafichua wahalifu katika maeneo yao ili kuepusha madhara yanayoweza kuwapata Wananchi.
Amewaambia Waandishi wa habari mkoani Dar es salaam kuwa jeshi hilo lina jukumu la kulinda raia na mali zao, hivyo ushirikiano wa Wananchi ni muhimu katika kufanikisha jambo hilo.
Katika tukio lililotokea tarehe 17 mwezi huu katika baa ya Lamax Sinza, mteja anayejulikana kwa jina la Alex korosso maarufu kama simba alimpiga risasi kijana aliyetambuliwa kwa jina la Gift Mushi kabla ya yeye kujipiga risasi shingoni na kufariki dunia papo hapo.
Kuhusu mtu aliyetekeleza mauaji katika eneo la Mbezi Makabe Kamanda Muliro amesema Jeshi la Polisi lipo kwenye hatua za mwisho ili kumfikisha mahakamani mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria.