Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAAJIRI WAASWA KUZINGATIA USALAMA NA AFYA KATIKA MAENEO YA KAZI


Na; Mwandishi Wetu – Dar Es Salaam
Waajiri nchini waaswa kuzingatia maswala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali, na madhara ya kiafya kwa kuwa na mazingira yenye usalama na ustawi kwa wafanyakazi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha Fujian Hexiawang na Kiwanda cha Lodhia Group of Companies vilivyopo Wilaya ya Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Akiwa katika ziara hiyo iliyolenga kufuatilia uzingatiaji wa sheria na kanuni za usalama na afya katika maeneo ya kazi Waziri Mhagama alieleza kuwa waajiri wote wanawajibu wa kuhakikisha masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi yanazingatiwa ili wafanyakazi waweze kutekeleza shughuli zao kwenye mazingira ambayo ni salama.

“Tulipokea malalamiko kuhusu kiwanda cha Fujian Hexiawang kinachozalisha nondo kuwepo kwa mapugufu katika mazingira ya utendaji kazi kwa wafanyakazi waliopo katika kiwanda hicho ambao walikuwa wakibeba vyuma chakavu na kuweka kwenye tanuri la moto (Jiko la kuyeyusha Vyuma chakavu) hali ambayo ilikuwa hatarisihi kwa wafanyakazi hao,” alisema Waziri Mhagama

“Serikali katika kuwajali wananchi wake kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) ilikutana na mwekezaji wa kiwanda hicho na walijadiliana pamoja kuona teknolojia bora ya kuwalinda wafanyakazi wa kiwanda hicho kwa kuwa na mtambo maalumu wa kubeba na kuweka vyuma chakavu kwenye tanuri la moto badala ya wafanyakazi kufanya kazi hiyo ambayo ilikuwa hatarishi kwao,” alieleza Waziri Mhagama

“Vilevile jukumu la mwajiri kugawa vifaa kinga kwa wafanyakazi ikiwemo maovaroli maalumu, vifunika uso, glovu, kofia ngumu n.k ili kulinda wafanyakazi katika mazingira ambayo ni hatarishi,” alieleza

Aliongeza kuwa lengo la kuzingatia usalama na afya mahala pa kazi ni kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na mazingira mazuri ya kazi na kiafya ili waweze kutekeleza majuku yao kwa weledi na ufanisi.

“Mnatambua kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa akihamasisha uwekezaji nchini ambao utazalisha ajira zaidi kwa vijana. Lakini kupitia uwekezaji huo serikali imekuwa ikihamasisha wawekezaji kufuata Sheria na Taratibu zilizopo nchini kwa kuzingatia usalama na afya za wafanyakazi katika kujenga uchumi wa nchi” alieleza

Katika kutekeleza hayo, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) imekuwa na jukumu la kuhakikisha maeneo ya kazi yanazingatia usalama na afya ya wafanyakazi nchini kwa kudhibiti, kusimamia utekelezaji na kuendeleza viwango imara vya usalama na afya kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, Waziri Mhagama alipongeza viwanda hivyo kwa kuzalisha nondo imara ambazo zimekuwa zikitumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa nchini ikiwemo Miradi ya Kimkakati (reli ya Kisasa ya SGR, mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere na Daraja la Tanzanite), Barabara na Vituo vya Afya vinavyojengwa katika maeneo mbalimbali.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Mhagama amewataka wafanyakazi watumie haki yao ya kutoa taarifa kuhusu majanga mbalimbali ambayo yanatokea katika maeneo ya kazi ikiwemo kuumia kwa mfanyakazi, ugonjwa au kifo kutokana na kazi ili hatua na taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Sambamba na hayo ameutaka Uongozi wa viwanda hivyo kufanya tathmini ya vihatarishi akitolea mfano vilipuzi ambavyo vimekuwa hatarishi kwa wafanyakazi waliopo katika maeno ya uzalishaji katika kiwanda hivyo.

“Tuliwapa miongozo ikiwemo kuweka utaratibu wa kubeba vyuma chakavu na kupeleka kwenye tanuri pamoja na kuweka mtu wa kuweza kutambua vyuma salama, alieleza

Waziri Mhagama ametaka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kuendelea kutoa elimu na mafunzo ya usalama kwa waajiri na wafanyakazi. Pia alihimiza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wafike katika viwanda hivyo na kutoa elimu na ufafanuzi juu ya masuala ya fidia kwa wafanyakazi ili waweze kutambua taratibu zikoje.

Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mhe.Abdallah Ulega alieleza kuwa ziara hiyo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, imekuwa ni faraja kwa wafanyakazi wa viwanda hivyo kwa kuwa wanatambua changamoto zao zitafanyiwa kazi kwa ufasaha.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Mhe. Hadija Ally alieleza kuwa maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri watahakikisha wanayasimamia na kuyafanyia kazi ili waweze kulinda maslahi ya wafanyakazi, kuhakikisha wanakuwa na mikataba na wanafanya kazi katika mazigira ambayo ni rafiki kwa lengo la kuimarisha ustawi wao.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda alisema kuwa Taasisi hiyo itaendelea kufanya kaguzi za kufuatilia utekelezaji wa usalama na afya katika maeneo ya kazi.

“OSHA itaendelea kushirikiana na wawekezaji, waajiri na wafanyakazi katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini ili kuhakikisha vihatarishi vinatambulia na kutengenezewa mikakati ya kidhibiti kwa ajili ya kuzuia madhara kwa wafanyakazi na mitambo iliyowekezwa,” alisema Mwenda


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com