WAZIRI MKENDA AENDELEA NA MKAKATI WA KUDHIBITI ONGEZEKO LA BEI YA MBOLEA


Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es Salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amewasili nchini akitokea nchini Morocco ambapo pamoja na mambo mengine katika ziara yake hiyo aliitembelea kampuni ya uuzaji wa mbolea ya OCP ili kuendelea na mkakati wa serikali katika kuhakikisha kuwa mbolea inapatikana kwa wingi nchini.

Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja katika bandari ya Dar es salaam tarehe 20 Julai 2021 Waziri Mkenda amesisitiza kuwa Serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha inadhibiti ongezeko la bei ya mbolea.

Amesema kuwa bei ya mbolea kwenye soko la Dunia imepanda kwa kiasi kikubwa hivyo serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa bei ya mbolea nchini inaendelea kuwa katika ustahimilivu wa bei huku juhudi zikiendelea za kuhakikisha bei ya mbolea inashuka bei.

Amesema kuwa uingizaji wa mbolea umeongezeka kwa kiasi kikubwa hapa nchini. “Hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wa mbolea nchini wanaohifadhi mbolea wakidhani bei itapanda, hilo hapana itashuka hivyo ni bora kuiuza mbolea hiyo mapema” Amekaririwa Waziri Mkenda

Waziri Mkenda amesema kuwa serikali haina kodi kwenye mbolea ila sehemu pekee ya gharama ilikuwa ni ucheleweshaji wa kushusha mbolea pamoja na bei ya soko la Dunia. “Sijasema kwamba bei ya mbolea itashuka sana maana bei imepanda Duniani” Amekaririwa Waziri Mkenda

Waziri Prof. Mkenda ameongeza kuwa Wizara yake tayari imefanya mazungumzo na Uongozi wa Bandari ya Dar es salaam ili kuhakikisha kuwa mbolea inapowasili bandarini inapewa kipaumbele ili iweze kupakuliwa kwa haraka na kuwafikia wakulima kwa wakati, “Kwa hili naomba niipongeze Bandari ya Dar es salaam mmeendelea kusimamia kwa ufasaha swala la upakuaji wa mbolea kwenye meli zinazowasili” Amesema

Ameongeza kuwa ili kuhakikisha changamoto za wafanyabiashara zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka tayari Serikali imeshatoa maelekezo ya Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) kuanza kutoa vibali vya kuuza mbolea ambayo imeshaingia nchini (Export Permit) badala ya vibali hivyo kutolewa ofisi ya Waziri wa Kilimo kama ilivyokuwa awali.

Ameongeza kuwa ili kuongeza ufanisi zaidi wa utendaji vibali hivyo vitatolewa kwa njia ya mtandao (Online) badala yake Ofisi ya Waziri wa Kilimo itakuwa na jukumu la kupewa taarifa ya utekelezaji wa utoaji vibali uliofanywa na TFRA.

MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
أحدث أقدم