WAZIRI NDAKI AMALIZA MGOGORO WA ARDHI RANCHI YA KAGOMA

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na viongozi na wataalam kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera na Wilaya ya Muleba kuhusu migogoro iliyopo kwenye Ranchi ya Kagoma na Mwesa ambapo ameagiza upimaji ufanyike katika eneo hilo ili kutatua migogoro iliyopo sasa ili wawekezaji waweze kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya kufugia mifugo na wananchi waendeleze shughuli zao za kiuchumi. Kikao hicho kimefanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Muleba.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi na wawekezaji waliopo kwenye Ranchi ya Kagoma kuhusu mgogoro wa ardhi ambapo ameagiza maeneo yaliyovamiwa na wananchi yapimwe ili wawekezaji waweze kubakiwa na eneo ambalo halitakuwa na mgogoro na kwamba baada ya kupimwa atakae vamia eneo la mtu atachukuliwa hatua.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifafanua jambo kuhusu upandaji wa malisho kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila (katikati) wakati walipokua wanakagua baadhi ya maeneo kwenye Ranchi ya Kagoma iliyopo wilayani Muleba Mkoa wa Kagera.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza jambo Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Prof. Faustine Kamuzora (katikati) wakati wa mkutano wa kutatua mgogoro kati ya wananchi na wawekezaji kwenye Ranchi ya Kagoma. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Prof. Peter Msoffe.

Wananchi na wawekezaji katika Ranchi ya Kagoma wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (hayupo pichani) wakati alipofanya mkutano kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi katika ranchi hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wataalam kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba, Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Kijiji cha Rutoro mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili hali ya migogoro kwenye Ranchi za Kagoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi na wataalam kutoka wizarani upande wa sekta ya Mifugo, sekretarieti ya mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba, Chama cha Mapinduzi na wawekezaji katika Ranchi ya Kagoma mara baada ya kumalizika kwa kikao kilichojadili hali ya migogoro kwenye Ranchi hiyo.

........................................................

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki ameumaliza mgogoro wa ardhi kati ya wananchi waliovamia kwenye vitalu katika Ranchi ya Kagoma na wawekezaji ambao wanamiliki vitalu hivyo.

Waziri Ndaki ameumaliza mgogoro huo leo (10.07.2021) baada ya kuwasikiliza wananchi na wawekezaji kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Rutoro wilayani Muleba Mkoa wa Kagera.

Akizungimzia kuhusu mgogoro huo, Waziri Ndaki aliwaeleza wananchi kuwa maeneo hayo waliyoyavamia ni mali ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ambayo tayari yalikuwa yameshakodishwa kwa wawekezaji wanaofanya shughuli za ufugaji hivyo walipaswa kuondolewa. Lakini kutokana na busara za Mhe. Rais Samia ameridhia eneo hilo lipimwe na wananchi wabakizwe kwenye vijiji vinne vilivyopo ambavyo ni Kijiji cha Rutoro, Byengeregere, Chobuheke na Mishambya vilivopo katika Kata ya Rutoro.

“Ninyi wananchi mnatakiwa kumshukuru sana Rais Samia kwa maamuzi yake ya kuwabakiza katika maeneo haya. Lakini niwasihi kuwa watulivu wakati wa zoezi la upimaji wa maeneo na kutoa ushirikiano kwa wataalam watakao kuja kutekeleza zoezi hilo,” alisema Waziri Ndaki.

Vilevile amewataka wananchi kutoendelea kuvamia maeneo mengine katika ranchi hiyo kwani wakifanya hivyo kwa sasa watachukuliwa hatua. Waziri Ndaki pia ametoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kuuza maeneo hayo wakati wao wenyewe hawajamilikishwa.

Pia kwa upande wa wawekezaji hao amewahakikishi kuwa zoezi hilo la upimaji wa maeneo halitaathiri shughuli zao za ufugaji kwa kuwa utawekwa utaratibu mzuri. Vilevile amewaeleza kuwa maamuzi hayo ya kupima maeneo na kuweka alama za mipaka yatasaidia sana kupunguza migogoro ya ardhi na kufanya pande zote kuishi kwa amani.

Katika mkutano huo yalitolewa malalamiko kuwa wafugaji wanalisha mifugo kwenye mashamba yao na kuwasababishia hasara. Kutokana na hilo Waziri Ndaki aliwaagiza wafugaji hao kuacha tabia hiyo kwani ni moja ya vitu vinavyosababisha tatizo la njaa kwa wananchi na kuleta migogoro baina ya pande zote mbili.

Vilevile wawekezaji wametakiwa kuhakikisha wanayatumia maeneo waliyopewa kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo. Aidha, uongozi wa wilaya ya Muleba umetakiwa kuweka utaratibu utakaotumika kuwaondoa wavamizi kwenye vitalu ambao wameingiza mifugo yao wakati hawajamilikishwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila amemuhakikishia Waziri kuwa maelekezo aliyoyatoa watakwenda kuyasimamia kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Kagera na uongozi wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO).

Kutokana na uamuzi uliochukuliwa wa kupima maeneo hayo kwenye ranchi ya Kagoma, wawekezaji na wananchi wote wameonesha mtazamo chanya kwani hata wao wenyewe hilo ndio wameliona ndio suluhisho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post