Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Tabora
WAZIRI wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda amewaonya baadhi ya viongozi wenye tabia ya kuingialia Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Mazao (AMCOS) huku akiwataka kuacha tabia hiyo mara moja.
Aidha, amesema ushirika sio idara ya serikali hivyo hauwezi kuongozwa kama idara kwakuwa mamlaka yake ina mipaka na hakuna kiongozi anayetakiwa kuingilia matumizi ya fedha wala kuzipangoa matumizi.
Waziri Mkenda ametoa agizo hilo (Jumamosi, Julai 3, 2021) kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika viwanja vya lipuli, Tabora, ambapo alisema kwa kiasi kikubwa serikali imepambana kurejesha mali mbalimbali za ushirika zilizokuwa zimeibiwa kupitia ushirika.
”Tumepambana sana na wabadhilifu kwenye ushirika na kurejesha mali mbalimbali zilizoibiwa kupitia ushirika hivyo kurudisha imani ya wanaushirika, na mali zao haziwezi kufanyiwa ubadhirifu wa aina yoyote.
Tutaendelea kusimamia ushirika kuhakikisha kwamba unaendelezwa kwa weledi, uwajibikaji na uwazi ili watu wengi wakubali kujiunga na ushirika kwa sababu unasaidia sana kunyanyua hali zao za kimaisha kwa kuwa ni hiari kujiunga hakuna kulazimishwa,”alisema.
Alieleza kuwa ushirika ni hiari na msingi wa kwanza duniani na kwamba ni kweli ushirika sio idara ya serikali hivyo hauwezi kuongozwa kama IDARA YA SERIKALI KWAKUWA mamlaka yake kwenye ushirika yana mipaka yake.
”Na hili ni muhimu kwa sababu kuna mahali ametokea kiongozi mmoja kaingia kwenye AMCOS anatoa amri toa shilingi milioni ishirini na tano hapa peleka kule, hatuna mamlaka hayo, ushirika ni hiyari ya wanaushirika
”Na hapaswi kupelekesha wana ushirika wanapaswa kujisikia kwamba ushirika ni mali yao, wasimame kidete, wasimamie shughuli zao bila kuingiliwa kinyume na taratibu zinazokubalika,”alisema.
Alisisitiza anasema hilo kwa sababu kuanzia Waziri wa kilimo (yeye), Mrajisi wa ushirika, wote lazima wajue mpaka upi wa kwao au si wao
”Mpaka sasa tunakwenda vizuri ukiacha hilo tukio mtu kwenda kutoa amri chukua hela za ushirika kutoka eneo moja kupeleka eneo ambalo ushirika huo hauhusiki nalo kwenda kujenga shule,
”shule ni jambo zuri lakini hakuna mamlaka ya kiongozi yoyote kwenda kuingia kwenye ushirika kuingilia fedha zao kuzipangia matumizi hayo yatafanywa na wanaushirika wenyewe ,”alisema.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin