Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Waziri Ummy Atoa Siku 7 Kwa Vyombo Vya Usalama Kuchunguza Vifo Vya Wanafunzi Watatu Mpwapwa


Nteghenjwa Hosseah, Mpwapwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu ametoa siku 7 kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchunguza vifo vya wanafunzi 3 waliofariki kwa kufunikwa na kifusi katika Shule ya Msingi Mbori, Kata ya Motondo Wilayani Mpwapwa.

Wakati huo huo Mhe. Ummy amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwaondoa Walimu wote wa shule ya Msingi Mbori kupisha uchunguzi unaondelea.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo wakati aliposhiriki kuaga Miili ya wanafunzi 3 waliofariki kwenye ajali ya kufukiwa na Mchanga katika shule ya Msingi Mbori tarehe 27.07.2021.

Akiwa shuleni hapo Waziri Ummy amelaani vikali Vitendo vya Walimu kuwafanyisha kazi siziso stahili za wanafunzi tofauti na ilivyoelekezwa kwenye Waraka wa Elimu bila Malipo No. 3 wa Mwaka 2016.

Amesema “ Hatukatazi mwanafunzi kufanya kazi zinazomjenga kama vile Stadi za kazi lakini sio kumfanya mwanafunzi kama Kibarua unawezaje kumwambia mtoto akachimbe mchanga wa kujengea au akaponde kokoto tena bila Uangalizi wa Walimu “ Alihoji

Katika Shule ya Msingi Mbori tumeleta sh. Mil.12 kwa ajili ya Ujenzi wa Choo na fedha za mchanga zimejumlishwa humo inakuwaje walimu watume watoto kwenda kuchimba mchanga wa mtoni,  kuna uzembe hapa umefanyika na tutachukua hatua.

Pia Waqziri Ummy aliwataka Wakuu wa shule zote Nchini na walimu wa ujumla kuacha kuwatumikisha wanafunzi wawapo shuleni na wazingatie Waraka wa Elimu bila Malipo no 3. wa mwaka 2016 ambao unatoa ufafanuzi wa kina wa jukumu la kila mdau wa Elimu.

“Jukumu la Ujenzi wa Miundombinu ya shule ni la Wazazi pamoja na Jamii inayozunguka na sio wanafunzi, Walimu na Kamati za shule mnatakiwa kuhamaisha Wazazi na jamii kujitolea kujenga miundombinu hiyo na sio kutumikisha wanafunzi” alisistiza Waziri Ummy.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mhe.Josephat Maganga  amesema watoto waliofariki kwenye ajali ya kufukiwa na kifusi shuleni hapo ni watatu ambao ni Isaya Lucas Hamis, Rehema Alex na Daud Enock Mchea na watoto wengine watano walijeruhiwa wametibiwa na kuruhusiwa kurejea majumbani kwao.

Tukio la Watoto kufukiwa na kifusi lilitokea Tarehe 27.07.2021 katika Shule ya Msingi Mbori iliyopo Kata ya Matomondo Wilayani Mpwapwa baada ya watoto hao kupewa kazi na walimu wao kuchimba mchanga kwa ajili ya ujenzi wa choo unaondelea shuleni hapo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com