WAZIRI WA KILIMO ATANGAZA MBOLEA MBADALA ZA DAP KUUZWA KWA BEI YA MSIMU ULIOPITA ILI KUWAPA AHUENI WAKULIMA
Wednesday, July 28, 2021
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imetangaza unafuu kwa wakulima kwa mbolea za kupandia aina ya NPS na NPS Zink ambazo zitauzwa kwa kiwango cha kati ya Shilingi 60,000 na 65,000 Mtawalia Jijini Dar es salaam.
Mbolea hizo ni mbadala wa mbolea za kupandia aina ya DAP ambayo imekuwa na bei kubwa kutokana na kupanda kwa bei ya mbolea hiyo kwenye soko la Dunia.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ametoa ufafanuzi huo Ofisini kwake Jijini Dodoma leo tarehe 28 Julai 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu muarobaini wa kadhia ya kupanda bei ya mbolea
Waziri Mkenda amesema kuwa mbolea hizo za kupandia aina ya NPS na NPS Zink ambazo ni mbadala wa mbolea aina ya DAP zimefanyiwa utafiti wa kitaalamu na kuonyesha matokeo mazuri Zaidi ya mbolea ya DAP kwa sababu zenyewe zimeongezwa virutubisho vya ziada ambavyo ni Salfa na Zink.
Waziri Mkenda amesema kuwa mbolea hizo zipo katika maeneo mbalimbali nchini na hivyo wananchi waendelee kuzitumia bila kuwa na wasiwasi wowote.
Waziri Mkenda amesema kuwa gharama hizo rafiki kwa mbolea zinazozalishwa na kampuni ya mbolea ya OCP ni matokeo ya ziara ya kikazi aliyofanya nchini Morocco ambapo alitembelea kiwanda hicho.
Kuhusu mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja (BPS), Waziri Mkenda amesema kuwa serikali iliamua kuufuta mfumo huo kwani haukuonyesha matokeo makubwa kama yalivyokuwa matarajio ya serikali.
“Tumeamua kuruhusu wafanyabiashara kuagiza bila mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja-BPS ambayo hata hivyo haitakuwa na kibali mpaka pale Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea nchini (TFRA) itakapotoa kibali baada ya ukaguzi kukamilika” Amekaririwa Mhe Mkenda
Kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni mengine ya mbolea ili kuona uwezekano wa kupunguza bei za mbolea ambazo zimekuwa kikwazo kwa wakulima.
Kwa upande wake Meneja wa Kampuni ya Mbolea ya OCP nchini Tanzania Dkt Mshindo Msolla amesema kuwa mbolea aina ya NPS na NPS Zink inauzwa kwa bei nafuu kuliko mbolea zingine hivyo ametoa mwito kwa wakulima kujitokeza kwa wingi ili kuinunua jambo litakalowarahisishia upatikanaji wa mbolea.
Amewaomba wakulima ambao wameshatumia mbolea hiyo katika mikoa yote nchini kutoa elimu kwa wakulima wengine ili kuona umuhimu wa mbolea ambayo bei yake ni nafuu na itarahisisha gharama za wakulima ambazo ni kubwa kwenye mbolea zingine.
Kwa upande wake Dkt Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI MLINGANO) Kilichopo mkoani Tanga amesema kuwa mbolea hizo zina virutubisho vya ziada ukilinganisha na mbolea zingine ambazo zinauzwa kwa gharama kubwa ambazo wakulima wameshindwa kuzihimili.
Amesema kuwa baadhi ya wakulima waliwahi kutumia mbolea hiyo tayari wameyaona matokeo mazuri katika mazao yao hivyo wanapaswa kuziamini mbola za NPS na NPS Zink kwani Taasisi ya utafiti wa kilimo-TARI imefanya utafiti katika kanda ya nyanda za juu kusini, Kanda ya mashariki, Kaskazini, Magharibi na kanda ya kati katika ikolojia zote saba za kilimo na kuyaona matokeo mazuri ya mbolea hizo.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin