Jamaa aliyetambuliwa kwa jina Joshua Kalama kwa sasa anapigania maisha yake hospitalini baada ya walinzi wa klabu moja Kajiado nchini Kenya kumvamia kufuatia kujaribu kutekeleza wizi kwa kutumia mabavu.
Akiwa amejihami na bunduki feki, jamaa huyo mwenye umri wa miaka 29, alikuwa amemshambulia mlinzi akijaribu kuingia ndani ya klabu hiyo.
Hata hivyo, mlinzi huyo hakuwa tayari kumruhusu kuinga ndani na hivyo mshukiwa alichomoa kile kilionekana kama bunduki.
Jamaa alimshtua mlinzi huyo akitumia bunduki hiyo bila kufyatua risasi, na alipotambua kuwa bunduki hiyo ilikuwa feki, mlinzi huyo pamoja na wenzake walimvamia mshukiwa kwa mangumi na mateke.
"Walimvamia jambazi huyo kwa mangumi na mateke na vifaa vingine vilivyokuwa karibu na kumuacha akigaragara kwa maumivu sakafuni," ilisema DCI.
Jamaa huyo aliokolewa na makachero kutoka mjini Kajiado ambao walimkimbiza katika hospitali iliyoko karibu kwa matibabu.
"Maafisa wetu kutoka Kajiado wasingelifika kwa muda, Joshua Kalama angelifariki kwa kutishia maisha ya mlinzi na bastola ambayo ilikuwa feki," iliongezea DCI.
Atakapopata nafuu, mshukiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya jaribio la wizi wa kimabavu kinyume cha kipengee cha 295 cha katiba.
Chanzo - Tuko News