Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Godwin Mollel
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Godwin Mollel amewataka wananchi kuipa umuhimu chanjo ya UVIKO-19 na kusema kuwa ni salama kwa afya zao.
Dkt. Mollel amesema hayo leo Jijini Dodoma kwenye Mkutano Mkuu wa wadau wa huduma za elimu ya afya kwa umma uliofanyika jijini Dodoma ambapo amesema wananchi hawapaswi kuogopa maneno yanayoendelea mitandaoni kuhusu chanjo hiyo kwani Serikali inawajali na kamwe haiwezi kuwaangamiza.
Mbali na hayo amesema Tanzania ni taifa la Mungu hivyo hatma yake iko mikononi kwa Mungu na kuwataka watanzania kuelekeza imani yao kwa Mwenyezi Mungu kumaliza wimbi la tatu la Ugonjwa huo.
Dk. Mollel ametumia nafasi hiyo kuwataka wadau hao wa huduma za elimu ya afya nchini,kuchapa kazi na kuwasihi waandishi kuzingatia maudhui yanayofaa kurusha kwenye vyombo vya habari.
"Msiogope yanayoendelea mitandaoni na kwenye vyombo vya habari ni kawaida tu, mambo yatakaa vizuri,,, Mkachape kazi hayo mengine mtuachie sisi Maronaldo wenu wao watakuja na wataondoka wakiwa wamefunga goli 0,,hali ya chanjo inaenda vizuri", amesema.
Katika kutoa elimu kwa umma aliwataka wadau hao kuwashirikisha watu maarufu, wasanii na viongozi wa dini ili kufikisha elimu kwa umma kuhusu umuhimu a chanjo ya Uviko 19 hasa katika sehemu za vijijini.
Aidha aliwataka wadau kutokujielekeza katika kufanya semina na makongamano na badala yake bajeti iliyowekwa itumike kuwawezesha wadau kuwafikia wananchi ili kutoa elimu ya afya kwa umma na chanjo ya Uviko 19.
Akitoa salamu kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na teknolojioa msemaji wa wizara hiyo Prisca Ulomi amesema wizara hiyo itashirikiana vizuri na wadau na makampuni ya simu kutoa elimu ya afya kwa umma kwa njia ya Tehama.