Na Magrethy Katengu - Dar es salaam
Wanzania wamehimizwa kupuuza maneno ya upotoshaji yanayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wanasiasa na watu maarufu viongozi wa dini kuhusu chanjo ya UVIKO -19.
Wito huo umetolewa leo na Balozi wa uhamasishaji wa chanjo ya UVIKO 19 ambaye pia mwenyekiti wa taasisi ya Wazalendo kwanza Steve Mengele Nyerere wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam ambapo amesema wapo watu wanahamasisha wananchi kutokuchanja kwa kueleza madhara ambayo siyo ya kweli.
"Ukifanya ubishi wa hili jambo fanya mwenyewe usiwashawishi wengine kaa kimya nyumbani kwako kwakuwa ukibainika unanashawishi watu wasichanje usijutie mdomo wako",alisema Steve.
Aidha amewahimiza vijana ambao ndio taifa la kesho kuwekeza nguvu zao katika kulisaidia Taifa kukua kiuchumi na sio kujiingiza kwenye makundi ya mitandao jamii inayolenga kuchafua serikali na kurudisha nyuma jitihada za Rais Samia ambaye amejielekeza katika kujenga uchumi na kusaida jamii kujikwamua katika lindi la umasikini.
Kwa upande wake Asha Baraka ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kujali wananchi wake Kwa kuwaletea chanjo na kuigawa bure kwa kila mmoja ili kusaidia hata wasio na uwezo wapate chanjo
Aidha Wazalendo kwanza wanasisitiza kuwa ugonjwa wa UVIKO -19 upo na unaua hivyo bi muhimu wananchi waliopo kwenye kundi la umri waliopewa kipaumbele kujitokeza na kuchanjwa kwa hiyari zao ili kunusuru maisha yao dhidi ya ugonjwa huo.