Salaam WanaMONDULI,
Nimefarijika leo kwamba nimekuwa mtu wa 972 katika wilaya ya Monduli kufanya Chanjo ya Covid 19 ya Janssen iliyozinduliwa Wilayani na Mkuu wetu wa Wilaya Mhe Frank Mwaisumbe tarehe 3 Agosti 2021.
Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza sana Wahudumu wa Afya wa Monduli na kote nchi nzima wanaohangaika kila siku kuhatarisha maisha yao ili kuokoa maisha ya wengi.
Kipekee, nimshukuru sana Rais wetu Mama SAMIA SULUHU HASSAN kwa jitihada kubwa sana ya kuhakikisha CHANJO hii ya Ugonjwa huu hatari inapatikana haraka iwezekanavyo kwa kuanza kusambaza Doses 1,050,000 nchi nzima.
Ni jitihada kubwa sana, hasa tukizingatia kwamba amekuwa RAIS ndani ya muda mchache sana. Kuna wachache wanajaribu kubeza, lakini tukumbuke hii siyo kazi rahisi hata kidogo, haswa ukizingatia msimamo wa nchi yetu ulivyokuwa dhidi ya JANGA hili hapo nyuma.
Dunia nzima imeamini kwamba njia sahihi na ya kisayansi ya kujikinga na Janga hili la Corona ni hizi CHANJO zilizothibitishwa na WHO (World Health Organisation). Ndugu na Marafiki zetu wengi wanafariki kila siku kwa janga hili la Covid-19, unadhubutu vipi kumshawishi mtu asichanje wakati haujampatia mbadala wowote wa kujikinga?
Naomba WanaMONDULI na WaTanzania wenzangu tuwapuuze, tukajilinde dhidi ya Janga hili, lakini zaidi tuendelee kumuunga mkono na kumtia moyo RAIS wetu Mama SAMIA SULUHU HASSAN.
Ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wengi wana matumaini makubwa sana kutokana na kasi kubwa aliyoanza nayo RAIS wetu kwenye Barabara Vijijini, Huduma ya AFYA kwenye Vituo Vipya vya Afya, Miradi ya MAJI, ELIMU kwenye Ujenzi wa Shule za Sekondari nk. Ni muhimu tuhakikishe ana AMANI MOYONI ili wananchi wengi waendelee kufaidika na UchapaKazi wake.
FREDRICK LOWASSA
MBUNGE - MONDULI
ARUSHA
Social Plugin