Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mwanaidi Ali Khamis
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto imewataka Maafisa ustawi na maofisa Maendeleo ya jamii kuwahamasisha wazee wote nchini kujitokeza kupata chanjo ya UVICO-19 kwa hiari yao katika vituo vinavyotoa chanjo hiyo.
Akiongea jana Jijini Dodoma Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mwanaidi Ali Khamis amesema kundi la Wazee ni miongoni mwa makundi yaliyopewa kipaumbele katika kutekeleza mpango huo wa kinga hivyo watoa huduma za afya wanapaswa kuwapa kipaumbele.
"Wazee ni kundi ambalo lipo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya UVIKO 19 nawasisitiza mtilie mkazo jambo hilo kwa sababu wazee ni tunu ya Taifa ambao wanastahili kulindwa na majanga mbalimbali ikiwemo kuimarisha ulinzi na usalama wa afya zao,"amesema na kuongeza;
“Kwa kuwa uzee na kuzeeka unaambatana na upungufu wa kinga ya mwili, Serikali inatoa wito kwa wazee wote nchini kujitokeza kwa wingi kutumia fursa ya chanjo ya UVIKO 19 inayotolewa bure katika vituo mbalimbali vilivyoainishwa”,amesema.
Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri huyo aliiasa jamii kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia miongozo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi na tiririka, kutumia vitakasa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka misongamano isiyo ya lazima.
"Tukifuata miongozo yote ya kijikinga na Corona tutafanikiwa na kuendelea na shughuli zetu za uzalishaji Kama waida bila kuwa na hofu ,"amesema.
Social Plugin