KAMATI YA USALAMA SHINYANGA YARUHUSU WAFANYABIASHARA KUCHUKUA DENGU ZAO


Mkuu wa Mkoa wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kamati ya Usalama Mkoa wa Shinyanga ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dr. Philemon Sengati (PhD) imewaruhusu wafanyabiashara wa mazao ya dengu kuchukua dengu katika maghala ya Chama Cha Ushirika (SHIRECU) kuanzia Jumatatu Agosti 30,2021.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa mkoa Dkt. Philemon Sengati kufanya kikao na wanunuzi wa dengu leo Agosti 28, 2021 kikao ambacho pia kimehudhuriwa na Kamati yote ya Ulinzi na Usalama mkoa,Wakuu wa wilaya, Waendesha ghala, Wakili wa Serikali, Mwanasheria wa Makampuni yaliyofungua kesi mahakamani na wawakilishi wa Makampuni ya ununuzi wa dengu.

Dkt. Sengati amesema amefanya maamuzi na kutoa agizo baada ya kupokea Waraka kutoka kwa Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda unaoelekeza kwamba mazao jamii ya mikunde ikiwemo dengu hayapo katika mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sasa.

Amesema Waraka huo umeondoa mfumo wa Stakabadhi ghalani kwa zao la dengu kwa mikoa inayolima dengu mpaka pale serikali itakapotoa maelekezo mengine.

“Jana Agosti 27,2021 nimepokea Waraka kutoka Wizara ya Kilimo wa tarehe 26.08. 2021 ukielekeza kuwa mazao jamii ya dengu hayatatumia mfumo wa stakabadhi ghalani na soko la bidhaa (TMX)”, amesema Dkt. Sengati.

“Hapakuwa na Waraka rasmi kutoka wizarani lakini baada ya kupokea Waraka nimekutana na wadau wa dengu na tumekubaliana utaratibu wa kuondoa dengu ghalani. Dengu hizi zitoke kwa utaratibu ambao hautaleta mgogoro”,amesema Dkt. Sengati.

Amesema kutokana na hali hiyo sasa Walanguzi watanunua dengu moja kwa moja kwa wakulima.

Vile vile Dkt. Sengati amewaomba wanunuzi hao kufuta kesi waliyoifungua mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kupinga amri ya kukamata mazao hayo ya Dengu kiasi cha tani 400 ambapo Wanunuzi hao wamekubali kuifuta kesi hiyo bila gharama yoyote kupitia kwa wakili wao Paul Kaunda.

“Tumekubaliana utaratibu wa kuondoa dengu ghalani uanze Siku ya Jumatatu hadi Ijumaa ambapo wanunuzi wa dengu watakuja kuchukua dengu zao bila masharti yoyote",amesema.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post