HAPA NDIYO GAMBOSHI.....SHUHUDIA HUDUMA ZA JAMII NA MAISHA YA GAMBOSHI



Shule ya sekondari Gamboshi iliyoko kijiji cha Gamboshi wilayani Bariadi mkoani Simiyu aliyoanzishwa mwaka 2019 kwa ajili ya kutoa elimu, kuondoa ujinga, kupiga vita masuala ya imani za kishirikina. (Picha zote na Costantine Mathias).
Shule ya sekondari Gamboshi iliyoko kijiji cha Gamboshi wilayani Bariadi mkoani Simiyu aliyoanzishwa mwaka 2019 kwa ajili ya kutoa elimu, kuondoa ujinga, kupiga vita masuala ya imani za kishirikina. 
Minara ya huduma za mawasiliano ya simu katika kijiji cha Gamboshi, kijiji ambacho kinasimuliwa kuwa kujihusisha na mambo ya ushirikina.
Mwalimu wa shule ya Msingi Gamboshi Kiriani January Lipembe akiandaa maada na zana za kufundishia wanafunzi wa darasa la saba shuleni hapo, wakati huu wa wa likizo kwa lengo la kuwaandaa wanafunzi kufaulu vizuri.
Muuguzi wa zahanati ya kijiji cha Gamboshi Pamela Mong'awi (mwenye kikoti cha njano) akitoa huduma kliniki na chanjo kwa akina mama na watoto wachanga waliofika katika zahanati hiyo kupata huduma za kimatibabu na upimaji.
Muuguzi wa zahanati ya kijiji cha Gamboshi Pamela Mong'awi (mwenye kikoti cha njano) akitoa huduma kliniki na chanjo kwa akina mama na watoto wachanga waliofika katika zahanati hiyo kupata huduma za kimatibabu na upimaji.
Zahanati  ya kijiji cha Gamboshi kwa ajili ya utoaji wa huduma za tiba, kijiji ambacho kinasifika kwa masuala ya ushirikina.
Zahanati ya kijiji cha Gamboshi kwa ajili ya utoaji wa huduma za tiba, kijiji ambacho kinasifika kwa masuala ya ushirikina.
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Gamboshi Agnes Alex wa kidato cha pili akichota maji katika kisima karibu na shuleni kwa ajili ya matumizi ya shule. (Picha zote na Costantine Mathias).





Na Costantine Mathias - Gamboshi 

Kutokana na masimulizi yaliyosambaa juu ya hali ya Maisha ya Gamboshi, huwezi kuamini kama kijiji hicho kinapata huduma za kijamii kama maeneo mengine kutokana na kuaminika kuwa ni kijiji cha Ushirikina.

Lakini ukweli uliopo ni kuwa huduma zote za kijamii zinazopatikana sehemu zingine, pia zinapatikana kijiji cha Gamboshi, ikiwemo huduma za afya, elimu, maji, umeme, mawasiliano pamoja na barabara.

Wenyeji wa kijiji hicho wanasema ni moja ya vijiji kama vijiji vingine licha ya kuaminika kwa masimulizi ya ushirikina jambo ambalo halina ukweli wowote kwa sasa kulingana na hali halisi iliyopo kijijini hapo.

Kiriani January Lipembe, mwalimu wa shule ya msingi Gamboshi anasema tangu aajiriwe, kwa miaka tisa sasa wanaishi na jamii vizuri na kwamba wanashirikiana kwa mambo mengi ikiwemo utoaji wa elimu.

‘’Walioko nje ya Gamboshi na maeneo mengine waondoe hofu, simulizi zilizokuwa zimesambaa hazifanani na uhalisia uliopo katika kijiji hiki…hata mimi mwenyewe kipindi naajiriwa sikuamini, lakini nilijipa moyo na nafanya kazi vizuri bila matatizo yoyote’’ ,anasema Lipembe.

Anaeleza kuwa dhana iliyokuwa imepandikizwa ilitokana na simulizi mbalimbali hasa nyakati za michezo ya mbina, kwani watu wengi walifika kwa ajili ya kushuhudia mamanju wakichuana kwa kushindana wakitumia madawa ya asili.

Anasema katika kijiji hicho kina huduma za elimu, afya, maji, dini, barabara na mawasiliano zinapatikana na wananchi wanashiriki katika shughuli za maendeleo pamoja na uchangiaji wa nguvu kazi.

"Dhana ya ushirikina na elimu ni vitu viwili tofauti, tunaendelea na utaoji wa elimu ili kuielimisha jamii ya eneo hili…hali ya kijiji ni tulivu, walimu hatuna hofu na tunashirikiana na jamii vizuri sana’’ ,anasema Lipembe.

Anasema jamii inashiriki katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu pia mwitikio wa wazazi kuchangia chakula shuleni ni mzuri kutokana na uongozi wa shule kwa kushirikiana na kamati ya shule huitisha vikao vya wazazi ili kujadili maendeleo ya shule pamoja na wanafunzi.

Anafafanua kuwa serikali ina mpango wa kuwasogezea wananchi huduma za maji karibu na maeneo yao, mradi ambao unatekelezwa na mamlaka ya maji vijijini na usafi wa mazingira (RUWASA).

Muuguzi wa zahanati ya Gamboshi, Pamela Mong’awi anasema hadhani kama yaliyosadikika bado yapo kwa sababu jamii imekuwa na mwamko wa kupeleka watoto kliniki na kuwapatia elimu.

Anasema ushirikina kila sehemu upo, lakini yaliyokuwa yamevumishwa katika kijiji hicho hayapo kabisa kwa sababu kijiji hicho kimekuwa na maendeleo kuzidi hata vijiji vingine jirani.

"Nina miaka saba nafanya kazi ya kutoa huduma za afya hapa,watu ni wakarimu na wanaushirikiano mkubwa, asilimia ndogo wanachangia maendeleo japokuwa bado wanaamini kazi ya kuleta maendeleo ni ya serikali’’ ,anasema Mong’awi.

Muuguzi huyo anasema uwezo wa zahanati hiyo bado ni mdogo kuhudumia wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani vya Yeya na Lulayu ambapo anaiomba serikali kuwaongeza majengo na watoa huduma.

Rebeka Thadeo mkazi wa Gamboshi anasema katika kijiji hicho hakuna tatizo lolote na maisha yanaendelea kama ilivyo kwa vijiji vingine na kwamba wananchi wanafanya kazi za kilimo, ufugaji na biashara ndogondogo.

"Ushirikina ulikuwa ni uvumi tu, nakumbuka nikiwa darasa la nne mwaka 1997 wakati tunasoma alikuwa amevumika mzee Gamboshi ambaye alikuwa mtemi wa watu wa Gamboshi na Jisesa…lakini leo hatuoni chochote’’, anasema Rebeka.

Wilson Heka mkazi wa kijiji hicho anasema huduma za elimu msingi, sekondari, afya (zahanati), maji, barabara, umeme, mawasiliano ya simu (minara ya simu) pamoja na barabara zinapatikana katika kijiji hicho.

Anasema elimu ilipoingia na baadhi ya imani potofu zikaanza kujifuta ikiwemo matumizi ya tiba asili na badala yake wagonjwa hupelekwa zahanati ya kijiji kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

‘’Neno la Mungu limetutoa kwenye imani potofu, jamii imeendelea kupata elimu na maisha yamebadilika, pia mwingiliano wa watu kutoka sehemu mbalimbali wametusaidia kuelimisha jamii’’, anasema Heka.

Mabula Magamula anawataka watu wasiokuwa wenyeji wa Gamboshi kuondoa hofu na dhana ya kuwa kijiji hicho ni cha wachai na bado kina imani za kishirikina.

Anasema kuwa, pia askofu mkuu wa kanisa wa Waadventista Wasabato (SDA) askofu Malekana anatokea katika kijiji hicho huku akisisitiza kuwa kijiji hicho kina wasomi wengi ambao wako maeneo mbalimbali.

"Askofu wa SDA, askofu Malekana anatoka Gamboshi, kuna wasomi wengi wanatoka hapa…wenye hofu waje kujifunza na kujionea hapa pia huduma zote za kijamii zipo kama maeneo mengine’’ anasema Magamula.

Mchungaji wa Kanisa la PAGT kata ya Gamboshi, Philipo Machibula anasema wanatumia maombi, mikutano na semina mbalimbali kuwaondoa watu katika imani potofu.

Anasema kijiji hicho kilijengeka kwa nguvu za giza na imani potofu ambapo kupitia maombi na kueneza imani ya dini watu wa eneo hilo wanaendelea kumwanini na kumwabudu Mungu.

"Imani potofu imebaki kwa watu wachache, lakini ishara tunaziona kuwa watu wamebadilika kutokana na kwamba wameacha masuala ya utamaduni ikiwemo michezo ya mbina…mabibi wengi waliosimulia mambo ya ushirikina sasa wameshabatizwa na kumwamini Mungu’’ ,anasema Machubula na kuongeza.

"Viongozi wa dini tunashirikiana kueneza neno la Mungu, na kila mmoja anakemea na kuomba kwa namna yake, tupo zaidi ya madhehebu matano na imani hizo kwa sasa zimeshaondoka na kubakia kama historia’’.

Anasema kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na taarifa nyingi za ukataji wa mapanga, lakini kwa sasa jamii imebadilika ulinzi shirikishi unafanyika na mhalifu akipatikana anafikishwa kwenye vyombo vya kisheria.

Diwani wa Kata ya Gamboshi Bahame Kaliwa anasema Gamboshi ya sasa ni ya amani, utulivu na mshikamano na wananchi wanafanya kazi kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Anawataka watu kufika Gamboshi kwa ajili ya kujionea maendeleo ya watu na vitu ili kuindoa dhana ya uchawi iliyokuwa imejengeka baina yao na watu wa mataifa.

‘’Gamboshi ya sasa ni ya amani, siyo kama Gamboshi ya zamani wala siyo kituo cha uchawi, ni mahali salama kama maeneo mengine…ni kama vijiji vingine nchini ambavyo vinapatiwa huduma za kijamii na serikali’’ ,anasema Kaliwa.

Anasema wanapambana kuleta maendeleo kijiji hapo na kata kwa ujumla ambapo miradi ya elimu, afya,maji, umeme na barabara imetekelezwa ili kuwarahisia wananchi kupata huduma.

‘’Tunapambana kuleta maendeleo wananchi katika kata yetu, Gamboshi ya sasa ni ya Maendeleo, kuna miradi ya visima vya maji inaendelea kutekelezwa, umeme umefika, barabara, ipo huduma za mawasiliano zipo, shule zipo na zahanati ipo’’, anasema Kaliwa.

Diwani huyo anasema wananchi wa Gamboshi wanaishi kwa furaha kama ambavyo binadamu wengine wanaishi katika maeneo yao huku akiwataka wasioanimi wafike kijiji hapo kujionea maendeleo na maisha ya wananchi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post