Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KABUDI AAGIZA UJENZI WA MAHAKAMA MANYONI UHARAKISHWE


Waziri wa Katiba na sheria Profesa Palamagamba Kabudi   baada ya kupokelewa  na Mkuu wa Mkoa  wa Singida  Dkt.Binilith  Mahenge.
Waziri wa Katiba na sheria Profesa Palamagamba Kabudi  akizungunza na viongozi wa taasisi mbalimbali za utoaji haki mkoani Singida.
Afisa Sheria Mkoa wa Singida Nasemba Mkambazi  akisoma taarifa za taasisi mbalimbali mkoani hapa za utoaji haki
Kikao kikiendelea.
Waziri Kabudi  akiwa  kwenye picha ya pamoja na viongozi  hao.
Waziri Kabudi akiteta jambo na Mkuu wa mkoa wa Singida  Dkt.Binilith  Mahenge.

**
Na Edna Malekela, Singida.

WAZIRI wa Katiba na Sheria Profesa Palamagamba Kabudi amesema masuala yote yanayohusiana na msingi wa haki za binadamu, demokrasia, maadili kwenye utumishi wa umma na utawala bora vimeainishwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tofauti na kejeli za wapinzani.


Profesa Kabudi alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa jana, alipokutana na viongozi waandamizi wa mahakama na wadau wa utoaji haki, wakati akikagua hali halisi ya mwenendo wa utoaji haki na utekelezaji wa sheria ya msaada wa huduma za kisheria iliyopitishwa na Bunge mwaka 2017.



Alisema kulingana na Ilani hiyo sura 6 ukurasa wa 161 hadi 181 inazungumzia ajenda ya Utawala Bora, Maadili kwenye Utumishi wa Umma, Rushwa, Demokrasia na Haki za Binadamu na kimsingi Wizara ya Katiba na Sheria ndio msimamizi katika kuhakikisha inapanua wigo kwa kuimarisha huduma hizo.



"Dhana na chimbuko la kuanzishwa kwa sheria ya msaada wa huduma za kisheria alisema ni utekelezaji wa takwa la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)," alisema Kabudi



Katika hatua nyingine, aliagiza watendaji wa mahakama mkoani hapa kuharakisha mchakato wa kuandaa eneo litakalotumika kwa mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni, ambayo pamoja na mambo mengine, inatarajia kujikita katika kushughulikia kesi za ujangili ili kuimarisha ulinzi wa mazingira


Hifadhi ya mto Kizigo uliopo kwenye msitu wa Rungwa wilaya ya manyoni mkoani hapa mbali ya kuwa na vivutio vya wanyama, pia mto huo ni moja ya chanzo muhimu kinachopeleka maji kwenye mto Ruaha ambao hutiririsha maji yake kwenye bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililopo Rufiji.


"Ujenzi wa mahakama hii ambayo itashughulikia kesi za ujangili, kulinda utajiri wa asili na mali za asili haukwepeki na upo kwenye mpango wa mwaka huu wa fedha, nataka kufikia Ijumaa muwe mmeainisha eneo la ujenzi wake na mmeshughulikia vibali vyote nitafika kukagua," alisema.


Aidha, alisema kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo msaada wa kisheria ulikuwa unatolewa kwa wale tu wenye makosa ya jinai, na makosa yenyewe ni yale ambayo adhabu yake ni kifo. Lakini sasa sheria hii mpya imeruhusu na kupanua wigo kwa fursa hiyo kutolewa kwa wananchi wote," alisema.



Kwa mujibu wa Ilani ya CCM pamoja na mambo mengine, imesisitizwa kwamba huduma hiyo ya msaada wa kisheria inapaswa kutolewa kwa kila halmashauri ya wilaya na ulenge zaidi makundi ya wanawake, watoto na wajane.


Kupitia ziara hiyo alikumbusha juu ya takwa la Ilani kuhusu kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa haki za kupata elimu, afya, maji safi na salama na nyinginezo huku akiwataka watu kutambua kwamba hizo pia ni haki za msingi za binadamu na si zile za kisiasa pekee ambazo zimezoeleka na wengi.


Pia aliitaka jamii kuwa na mtazamo chanya katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kujitokeza na kutoa ushahidi ili kurahisisha mwenendo wa mashauri hayo.


Akizungumzia suala la uendeshaji wa mashauri kwa kutumia lugha ya Kiswahili, Profesa Kabudi kupitia ziara hiyo alisema kwa sasa wapo kwenye hatua ya kutengeneza kamusi ya kiswahili cha kisheria itakayotafsiri sheria mbalimbali.


"Lugha hii ni fahari kwa taifa, na lengo hasa la kuendelea na hatua ya kutengeneza kamusi na kitabu cha kiswahili cha kisheria ni kuongeza 'access to justice' na tunatarajia mpaka ifikapo Juni 2022 kanuni za sheria mbalimbali zitakuwa zimetafsiriwa," alisema.


Katika hatua nyingine, Profesa Kabudi alionyesha kusikitishwa na namna watumishi walio wengi 'kubananga' (kuharibu) lugha ya kiswahili na kujikuta wakiingiza na kutumia ofisini lugha za mitaani zisizo na fasihi stahiki.


"Nimekasirika, nimefadhaika, nimeghadhabika kuona ndani ya serikali baadhi ya watumishi wameanza kupoteza umahiri wa kuandika kiswahili cha kiserikali na badala yake kinachotumika zaidi ni kile cha mtaani. Napenda ifahamike serikali ina kiswahili chake," alisisitiza na kuongeza;


Miaka ya nyuma ilikuwa mtumishi hawezi kupanda daraja bila ya kufaulu mtihani wa kiswahili kigumu uliotungwa na chuo cha utumishi wa umma magogoni..ni lazima tuanze kujifunza na kuandika nyaraka na miongozo kwa kutumia kiswahili cha serikali.


Awali, Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Mkoa wa Singida, Nasemba Mkambazi, alisema miongoni mwa changamoto zinazokabili sekta ya utoaji haki mkoani hapa ni kuwepo kwa Mahabusi wengi katika baadhi ya magereza.


Suala lingine ni kesi nyingi za ukatili wa kijinsia kama zile za ubakaji, ulawiti na kuwapa mimba wanafunzi kukosa ufanisi kutokana na kupata ushirikiano mdogo kwa kukosa mashahidi wa kesi.


Pia Kazen alisema changamoto kama kutokuwepo kwa Mahakama Kuu ndani ya mkoa, uhaba wa vitendea kazi na watumishi wanaohusika na utoaji wa haki jinai, na baadhi ya wilaya kukosa mahakama za wilaya ni pigo na hali hiyo inafifisha ustawi wa utoaji haki.


Waziri Kabudi baada ya kukutana na viongozi waandamizi mkoani hapa anatarajia pia kwa nyakati tofauti kukutana na viongozi na watumishi wote wanaohusika na utoaji haki jinai kwenye wilaya za Ikungi, Iramba, Singida, Mkalama na Manyoni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com