Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida Stella Mutabihirwa
Na Edina Malekela - Singida.
Mwalimu wa shule ya Msingi Misuna iliyopo katika Manispaa ya Singida anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumbaka Mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka (13) anayesoma darasa la sita katika shule hiyo.
Akitoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida Stella Mutabihirwa amesema tukio hilo limetokea usiku waAgosti 1,2021.
"Baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za kuhusu tukio hilo lilifanya uchunguzi na kubaini kuwa mtoto huyo ambaye jina lake limehifadhiwa alibakwa na mwalimu wake anayeitwa Alphonce Festo mwenye umri wa miaka (26) Mnyaturu ambapo usiku huo akiwa nyumbani kwake huko katika Mtaa wa Salimini alifanya tukio hilo",amesema.
Kamanda alisema mbinu aliyotumia mtuhumiwa kufanya tukio hilo ni kumhadaa binti huyo kwa kumuahidi kuwa atamuoa ambapo atakuwa na maisha mazuri jambo lililopelekea kufanya kitendo hicho.
Jeshi la Polisi bado linamshikilia Mwalimu huyo wakati taratibu za kumfikisha Mahakamani zinaendelea na tayari jalada la kesi hiyo limefikishwa kwa mwanasheria na hali ya afya ya mwanafunzi huyo inaendelea vizuri na anaendelea na masomo.
Aidha Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Singida kuachana na vitendo vya ubakaji kwani vitendo hivyo ni vya kikatili ambapo husababisha madhara mbalimbali kwa mtu kama vile magonjwa na kuathirika kisaikolojia ama kufa kabisa.
Social Plugin