Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MCHUNGAJI ALIYEZIKWA AKIWA HAI AKISEMA 'ATAFUFUKA KAMA YESU' AKUTWA AMEKUFA KABURINI

Mchungaji wa kanisa la Zion nchini Zambia James Sakara (22), aliyewaomba baadhi ya waumini wake wamchimbie kaburi na kisha wamzike akiwa hai kwa madai ya kwamba baada ya siku tatu angefufuka kama Yesu, amekutwa akiwa amefariki dunia.

Awali kabla ya maamuzi ya kuzikwa akiwa hai, baadhi ya waumini wake walimkataza kufanya ujinga huo lakini baadaye, walijitokeza waumini wake watatu ambao waliamini madai yake ya kwamba angefufuka ambao walimsaidia kuchimba kaburi lenye kina kirefu, kufunga mikono yake na kumzika akiwa hai.

Inaelezwa kwamba kabla ya kuzikwa aliwaambia waumini wake maneno haya.

"Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi," alisema mchungaji huyo.

Imeelezwa kuwa mara baada ya kumkuta amefariki dunia, waumini hao walianza kumfanyia maombi ya kumfufua tena jambo ambalo halikuwezekana.

Hadi sasa Jeshi la Polisi nchini humo linaendelea kuwashikilia waumini waliomsaidia kumzika akiwa hai mchungaji huyo.

Inaelezwa kuwa Mchungaji Sakara ambaye alikuwa mwenye umri wa miaka 22 alikuwa anajiamini kupita kiasi katika uwezo wake wa kuiga ufufuo wa Yesu Kristo.

"Hivyo kwake, haikuwa jambo la kupuuza wito huo kwa waumini wake, maana tayari alishajijengea mazingira makubwa ya imani baina yake na waumini na hata yeye mwenyewe,"amesema Daudi Chawezi  mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Amesema, nguvu aliyokuwa nayo ya ushawishi, Mchungaji Sakara ndiyo iliweza kuliingia kusanyiko la waumini wake na kuamini kuwa, angeweza kufufuka siku ya tatu kama Mwana wa Mungu miaka elfu kadhaa iliyopita.

"Ni jambo la kushtua sana, kwani badala ya kufufuka baada ya siku tatu, Mchungaji Sakara alikutwa amekufa na washiriki wa Kanisa la Sayuni waliotamani kuona kiongozi wao anatimiza ahadi yake ya kufufuka ndani ya siku tatu,"ameongeza.

Hata hivyo, baada ya kuona mwili wa kiongozi wao ambaye amekufa haufufuki,waumini wengine wa kanisa walijaribu mfululizo wa mazoezi ya kiroho ili kumfufua, lakini haikufanikiwa hadi sasa.

Ingawa, baadhi ya waumini wa Sakara walipuuza maono hayo ya Mchungaji wao, walikwamishwa na nguvu kubwa ya viongozi wa juu kanisani ambao walisisitiza lazima ahadi hiyo itimizwe.

James Sakara anaondoka duniani akiwa amemuacha mke wake akiwa mjamzito na waumini ambao hawajui hatiama yao iwapo mamlaka zitaanza kupita nyumba baada ya nyumba ili kufanya uchunguzi.

 Pengine imani potofu kutoka kwa Mchungaji huyo zinaweza kuingia katika rekodi za baadhi ya watumishi wa Mungu barani Afrika ambao wamekuwa wakimchezea Mungu kupitia makanisa.

Ni hivi karibuni tu walijitokeza baadhi ya wachungaji wenye vituko vingi wakiwemo waliodai kuwa wana namba ya simu ya Mungu ambayo wakipiga inaweza kuwaponya maelfu ya watu aina zote za magojwa na mateso.

Miongoni mwao ni Mchungaji wa Zimbabwe, Paul Sanyangore (32) ambaye alidai kuwa na namba ya Mungu na anaweza kumpigia simu haraka na kuzungumza naye mbele ya mkutano wake muda wowote.

"Nina kituo cha moja kwa moja na Mungu, kwa kweli nina namba yake na ninaweza kumpigia wakati mahitaji yanapotokea,"alinukuliwa hivi karibuni akieleza katika moja ya mahubiri yake.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com