Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AONGOZA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA ELIAS KWANDIKWA USHETU


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali na itatekeleza mipango yote iliyoachwa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, marehemu Elias Kwandikwa.

Amesema kuwa Serikali itaenzi mipango yake na itahakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni katika Jimbo la Ushetu zinatekelezwa kama alivyoahidi.

Ameyasema hayo leo alipomuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika maziko ya marehemu Kwandikwa kijijini kwao Butibu, Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Aidha,Majaliwa amewataka Watanzania, wana-Shinyanga na wana-Ushetu waenzi mambo yote mazuri yaliyoachwa marehemu Kwandikwa.

“Tumepoteza kiongozi aliyekuwa anaongoza majeshi yetu, amefanya kazi nzuri sana katika kipindi chote cha uhai wake alipokuwa anaitumikia Serikali; marehemu alikuwa mwadilifu, muwajibikaji na aliyefanya kazi kwa weledi mkubwa,”amesema.

Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Mawaziri, Naibu Mawaziri na Wabunge, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa George Simbachawene amesema marehemu Kwandikwa alikuwa ni kiongozi ambaye alitekeleza majukumu yake sawasawa na alihakikisha matokeo yanaonekana.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Faraji Mnyepe amesema marehemu Waziri Kwandikwa ameondoka wakati wizara ikiwa inamuhitaji kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka. “Marehemu Waziri Kwandikwa alikuwa ni kiongozi mwenye upendo wa hali ya juu na alikuwa mtenda haki kwa kila mtu,”alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo amesema marehemu Waziri Kwandikwa alikuwa ni mtu wa kipekee, msikivu na mnyenyekevu.

Alisema kuwa, marehemu Waziri Kwandikwa, alikuwa ni mwepesi wa kujifunza mambo ya kijeshi na alilisaidia jeshi kwa kadri ya uwezo wake katika kipindi chote alichokuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

“Alikuwa ni kiongozi asiyependa kukaa muda mwingi ofisini bali aliwatembelea makamanda maafisa katika maeneo yao ya kazi ili kuona utendaji kazi na changamoto zinazowakabili,”alisema.

Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Daniel Chongolo alisema marehemu Waziri Kwandikwa ameacha pengo kwani katika kipindi chote amekuwa na mchango mkubwa ndani ya Serikali, CCM na wananchi wa ushetu na Watanzania kwa ujumla.

“Tumepoteza kiongozi hodari, mahiri na CCM tumepoteza mtu aliyekipenda chama kwa moyo mkuu. Mwenyezi Mungu aendelee kuwa mfariji kwa familia, wana-Ushetu, wana-Shinyanga na Watanzania kwa ujumla,”amesema.

Awali, Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi na Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki Kahama, Askofu Ludovick Joseph Minde amesema marehemu Waziri Kwandikwa alikuwa ni mnyenyekevu, mwenye busara, hekima na mpenda maendeleo.

Aidha, Askofu Minde aliongeza kuwa marehemu Kwandikwa alikuwa mfadhili mkubwa katika maendeleo ya kiroho na kimwili.

Marehemu Waziri Elias Kwandikwa alizaliwa Julai 7, 1966 wilayani Kahama, Shinyanga na alifariki Agosti 2, 2021 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com