Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi Mhe. Ummy Mwalimu
Na Josephine Charles - Kahama
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi Mhe. Ummy Mwalimu ametoa siku 14 kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zipo chini ya asilimia 25 ya kuboresha hali ya Lishe nchini kujieleza ni kwanini wasichukuliwe hatua.
Ametoa maagizo hayo kwenye Mkutano wa Tathmini ya Utekelezaji wa Mkataba wa Lishe Nchini ambao umefanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga.
Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni pamoja na Shinyanga Manispaa, Tarime,Musoma,Tabora,Buhigwe,Sikonge,Chato,Kasulu Dc,Itigi,Handeni na Ileje.
Akizungumza katika Mkutano huo Mkuu wa Kitengo cha Lishe Ofisi ya Rais Tamisemi Bw. Mwita Waibe amesema tafiti zinasema watoto Millioni 151 Duniani wamedumaa,wakati Afrika watoto Millioni 59 sawa na asilimia 39 wamedumaa na kwa Tanzania watoto Milioni 3 Kati ya Milioni 9 wamedumaa wakati kiwango cha Udumavu Tanzania ni asilimia 31.8.
Amefafanua kuwa Udumavu huathiri ukuaji wa mwili na akili lakini pia Udumavu unaweza kurekebishwa ndani ya siku 100 za makuzi na Maendeleo ya watoto.
Ameongeza kuwa Takwimu zinaeleza kwamba kwa Darasa Lenye wanafunzi 45 nchini Tanzania wanafunzi 14 hawawezi kufundishika na iwapo Udumavu hautapungua Hadi 2025 Taifa linakadiriwa kupoteza kiasi cha Shilingi trillioni 39 sawa na Shilingi trillioni 3.5 kwa kila mwaka.
Aidha Mkutano huo umehudhuriwa na Wakuu wa Mikoa yote Nchini,Makatibu Tawala wote Nchini,Waganga Wakuu wa Mikoa yote Nchini,Maafisa Lishe wa Mikoa yote Nchini,Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana,kazi na Ajira ambaye pia Ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi pamoja na wadau wengine wa Lishe nchini.
Lengo la Mkutano huo kufanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Kahama ni kwa sababu Manispaa hiyo ilishika nafasi ya kwanza kwa ukusanyaji Mapato nchini,hivyo wamepelekwa kujifunza namna ambavyo wamefanikiwa ili wakatekeleze kwenye Maeneo yao ya kazi.