Na Dinna Maningo,Tarime
Afisa Utumishi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoani Mara Pius Sayayi amesema kuwa halmashauri ilitenga milioni 100 kutengeneza magari matano mabovu na kati ya fedha hizo ni milioni 22 pekee ndiyo zimelipwa na zingine milioni 78 hajui mahali zilipo.
Sayayi alisema hayo mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo wakati alipotakiwa na Mwenyekiti wa halmashauri ambaye pia ni Diwani kata ya Nyakonga Simion Samwel (CCM) kueleza sababu za magari kutotengenezwa licha ya halmashauri kutenga milioni 100 mwezi Februari,2021 kutengeneza magari mabovu.
Mwenyekiti huyo alimtaka kujibu swali hilo ambalo liliulizwa na Diwani wa Kata ya Nyarero John Muhabasi aliyetaka kufahamu kwanini Mhandisi ujenzi Ernest Maungo hana gari wakati madiwani waliagiza apewe gari ili kumrahisishia kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo na alipewa gari.
Muhabasi alisema kuwa anashangazwa Mhandisi ujenzi Maungo kudai mbele ya mkuu wa mkoa wa Mara Ally Hapi aliyekuwa Tarime kwa siku tatu wiki iliyopita kwenye halmashauri hiyo kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi,kwa kile alichodai kuwa sababu ya miradi mingi kuwa mibovu ni kutokana na yeye kukosa gari la idara ya ujenzi ili kufuatilia na kukagua miradi.
Afisa Utumishi huyo alisema kuwa halmashauri ina magari 20,katika kuboresha kitengo cha magari kilimpatia yeye kusimamia utengenezwaji wa magari matano yaliyotengewa fedha milioni 100 tangu mwezi Febuari mwaka huu.
"Magari matano yalipelekwa TAMESA Musoma ili kutengenezwa,milioni 16 ziliweza kulipwa kama gharama ya kutengeneza gari la idara ya kilimo na million 6 kutengeneza gari la idara ya Afya ambazo tulizituma TEMESA lakini wao wakasema hawajaziona fedha hizo ambapo lilikuwa ni tatizo la kimfumo na zimeshalipwa lakini fedha zingine milioni 78 mimi sijui ziko wapi", alisema Sayayi.
Diwani wa kata ya Nyansicha Samwel Muhono (CCM) alisema "Mtaalamu anaposema hajui pesa ziko wapi ndiyo tunataka tujue ziko wapi milioni 78? sasa yeye amesema anajua ni milioni 22 ndiyo zimelipwa TEMESA tunamuomba Mkurugenzi afuatilie ajue hizo fedha ziko wapi !"alisema Muhono.
Diwani wa kata ya Kwihancha Ragita Ragita (CCM) alisema "hata mimi nilishamuomba mhandisi anitembelee kwenye kata yangu kuna miradi ya ujenzi maboma 12 na hajaja,je nikweli hana gari?je nikweli alikabidhiwa gari?",alihoji Regita.
Diwani wa kata ya Regicheli John Bosco (CCM) alisema "huu ni utovu wa nidhamu kama mtaalamu unadanganya mbele ya RC huna gari unasema uongo na ndiyo maana hata kwenye makablasha haya wanaandika uongo uongo tu na kusema uongo ni kosa na ni dhambi kwanini useme uongo na ni kiongozi wa idara!", alisema Bosco.
Diwani wa kata ya Pemba Ngocho Wangwe aliongeza kusema"tuliomba taarifa ya matengenezo ya magari kiasi kilichotumika na kilichobaki katika kikao cha kamati ya ujenzi na kwanini magari hayo bado yako TEMESA na yalitengewa fedha milioni 100 lakini hayajaja tumeomba kikao kijacho watuletee taarifa hiyo",alisema Wangwe.
Akijibu swali la Diwani Ragita aliyetaka kufahamu kuwa ni kweli mhandisi hana gari ?je alikabidhiwa gari ?.Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Simion Samwel alisema kuwa mhandisi ujenzi alikabudhiwa gari lenye namba za usajili SM 5241 na maandishi yapo.
Alisema kwamba amekwazika mhandisi huyo kutamka mbele ya RC Hapi kuwa hana gari la kutembelea miradi na gari lilitengenezwa na akakabidhiwa na sababu ya kupewa gari ni ufatiliaji wa miradi ambayo mingi imejengwa chini ya kiwango licha yakuonyesha gharama kubwa za ujenzi ikiwemo miradi ya fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii(CSR) zinazotolewa na Mgodi wa dhahabu wa Noth Mara ambao kwa sasa unamilikiwa na kampuni ya Barrick .
"Tunamshukuru RC kuja Tarime siku tatu kutembelea miradi ambayo madiwani tumepiga sana kelele juu ya matumizi mabaya ya fedha za miradi na amejionea hali halisi,tatizo wataalamu huwa wanatudanganya kwenye taarifa zao,gari zote zilizokwenda kwenye matengenezo haijarudi hata moja nataka mkurugenzi wa halmashauri afuatilie hayo magari kwanini hayajarudi na fedha ziko wapi na tuje tupewe taarifa kikao kijacho", alisema Samwel.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Solomon Shati aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo aliwaomba madiwani wampe muda ili afatilie kwakuwa yeye ni mgeni na hajui chochote na kuahidi kukagua miradi yote ya halmashauri na taarifa ataitoa katika vikao vijavyo.