Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKAGUZI WA NDANI ALAUMIWA KWA KUSHINDWA KUFANYA UKAGUZI,AJITETEA HAKUPEWA UWEZESHO OFISI YA DED


Na Dinna Maningo,Tarime

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoani Mara wameeleza kuchukizwa kwa kitendo cha wataalamu akiwemo Mkaguzi wa ndani kutotekeleza maagizo yanayotolewa kwenye vikao vya Baraza hali inayosababisha kuwepo kwa changamoto nyingi zikiwemo za matumizi mabaya ya fedha katika miradi ya maendeleo.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa kata ya Nyakonga Simion Samwel  alisema kuwa maelekezo wanayokuwa wakiyatoa kwa wataalamu wa halmashauri iwapo yangezingatiwa halmashauri hiyo isingekuwa na changamoto nyingi zikiwemo za miradi ya ujenzi kutokamilika kwa wakati.

Mwenyekiti huyo aliyasema hayo kwenye kikao cha Madiwani baada ya kueleza kuwa Februari,2021walimpa maelekezo Mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Dismas Wagoma, ikiwa ni pamoja na kukagua miradi yote ya halmashauri na kutoa taarifa kama matumizi ya fedha katika miradi ya maendeleo yamefanywa kwa kuzingatia mipango kazi na bajeti iliyoidhinishwa lakini hadi sasa hajakabidhi ripoti ya ukaguzi.

"Ingekuwa maelekezo tunayotoa kwa wataalamu wetu yanazingatiwa haya tunayokuwa tukijadili na kulalamikia yasingekuwepo,Madiwani wanatoa hoja zao kila mara lakini hazifanyiwi kazi! Mkaguzi wa ndani tulimpa maelekezo akague miradi ikiwemo ile inayojengwa kwa fedha za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) lakini hadi leo hajatupatia ripoti", alisema Samwel.

Diwani wa kata ya Bumera Deogratius Ndege alisema kuwa halmashauri inakusanya mapato yatokanayo na mifugo kupitia minada lakini kata nyingi hakuna majosho, na limekuwa likijadiliwa kila mara  lakini hakuna utekelezaji licha ya halmashauri hiyo kuwa na vyanzo vingi vya mapato .

Mkaguzi wa ndani wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Dismas Wagoma alikili mbele ya Baraza la Madiwani kuwa ni kweli aliagizwa kufanya ukaguzi wa miradi,na kwamba alifanya ziara kwa kushirikiana na baadhi ya wataalamu lakini wakiwa kazini wakiendelea na majukumu walikwama kuendelea na kazi baada ya kuomba uwezesho ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri hiyo lakini hakupewa fedha.

"Nilifanya ziara mimi kama mimi nikatafuta wataalamu akiwemo mkaguzi wa ndani kutoka halmashauri ya mji Tarime tukaanza kazi lakini tukiwa kazini tukakwama tukakosa pesa nikaomba uwezesho ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri lakini sikupata! nikiwezeshwa fedha ntakamilisha ripoti yangu imebaki kazi ndogo ili ikamilike", alisema Wagoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Solomon Shati alisema kuwa kama pesa ndiyo kikwazo ofisi yake itamlipa pesa yeye na wakaguzi wenzake na wiki ijayo wataanza kazi ya ukaguzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com