Mvulana wa miaka 17 alikamatwa na maafisa wa polisi Ijumaa, Agosti 13 baada ya kuripotiwa kumpiga babake hadi kumuua. Mvulana huyo ambaye alikuwa mtahiniwa wa Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) alihojiwa kuhusiana na kifo cha babake baada ya mashuhuda kumtuhumu kumpiga kwa kifaa butu.
Maafisa wa polisi wakiwa wamebeba mwili. Kulingana na ripoti ya polisi, maafisa kutoka kituo cha Nandi Hills walipata habari kwamba mvulana huyo alimshambulia babake kufutia mzozo wa usajili wake katika kidato cha kwanza.
Iliripotiwa kuwa baba huyo mwenye umri wa miaka 42 alivamiwa na mwanawe ambaye alitaka kujua ni kwa nini alikosa kumsajili katika shule ya karibu na nyumbani.
Mashuhuda walidai kuwa mabishano yalizidi na mvulana huyo aliripotiwa kumgonga babaake kichwani na kumuacha akiwa amepoteza fahamu.
Mzee huyo alipata majeraha mabaya kichwani yaliyosababisha kifo chake.
OCPD wa Nandi Mashariki, David Nyabuto, alisema marehemu alikimbizwa katika hospitali ya Meteitet na majirani ambapo alipata huduma ya kwanza na baadaye kuhamishiwa hadi hospitali ya Kaunti ya Kapsabet kwa matibabu zaidi.
"Jumatano asubuhi, Agosti 11, alipelekwa katika hospitali ya Kaunti ya Kapsabet, lakini aliripotiwa kukata roho akiendelea na matibabu," OCPD iliiambia The Standard. Ripoti ya madaktari ilionesha kwamba alipoteza damu nyingi.
Kijana huyo alizuiliwa kwa mahojiano zaidi huku polisi wakiendeleza uchunguzi.
Chanzo - TUKO NEWS
Social Plugin