Mahindi yakikatwa
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema litafanyia uchunguzi suala tukio la Wafanyakazi wa TANESCO kufyeka mazao katika shamba la Mkulima wa Tinde wilaya ya Shinyanga kwa kile kinachodaiwa kuwa amelima katika njia ya umeme ili kubaini iwapo kilimo hicho kimefanyika kwa kuzingatia umbali salama.
Taarifa hiyo ya TANESCO Makao Makuu imesema TANESCO inaendelea kutoa Rai kwa wananchi kutokufanya shughuli za kibinadamu au kiuchumi karibu na miundombinu ya umeme na kwamba wananchi wanatakiwa kuzingatia umbali salama kutoka katika miundombinu ya umeme.
SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO)
UFAFANUZI KUTOKA KATIKA VIDEO IKIONESHA WAFANYAKAZI WA TANESCO WAKIKATA MAZAO
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kutolea ufafanuzi taarifa kutoka katika video clip ya Agosti 19, 2021 ikionesha Wafanyakazi wa TANESCO wakikata mazao eneo la Tinde mkoani Shinyanga.
Eneo hilo zinapita njia kuu za kusafirisha umeme mkubwa za msongo wa kilovoti 220 kutoka Shinyanga hadi Buzwagi na kilovoti 132 kutoka Shinyanga hadi Tabora.
TANESCO inaendelea kutoa Rai kwa wananchi kutokufanya shughuli za kibinadamu au kiuchumi karibu na miundombinu ya umeme.
Aidha, wananchi wanatakiwa kuzingatia umbali salama kutoka katika miundombinu ya umeme, ambapo umeme wa msongo wa kilovoti 220 umbali unaotakiwa ni mita 60, mita 30 kutoka katikati ya nguzo kuelekea kushoto na mita 30 kuelekea kulia.
Kwa umeme wa msongo wa kilovolti 132 umbali unaotakiwa ni mita 40, mita 20 kutoka katikati ya nguzo kuelekea kushoto na mita 20 kutoka katika ya nguzo kuelekea kulia.
Umbali huu umewekwa kitaalamu kwa ajili ya usalama wa raia pamoja na mali zao, lakini pia usalama wa miundombinu ya umeme ambayo Serikali inatumia fedha nyingi kuwekeza.
TANESCO itafanyia uchunguzi suala hili ili kubaini iwapo kilimo hicho kimefanyika kwa kuzingatia umbali salama kama ulivyoainishwa hapo juu.
Imetolewa na:-
Ofisi ya Uhusiano
TANESCO Makao Makuu
:Soma pia
Mahindi yakikatwa
Jana usiku Alhamis Agosti 19,2021 video clip inayoonesha watu wanaodaiwa kuwa ni wafanyakazi wa TANESCO ilisambaa mtandaoni ikionesha wakikata kata mazao ya mkulima wa Tinde anayedaiwa kulima kwenye njia ya umeme.
Kwa mujibu wa mmiliki wa shamba hilo lililofyekwa mazao yake, Hemed Rashid amesema aliamua kulima mazao hayo yakiwemo Mahindi, nyanya, mbogamboga na matikiti kufuatia kile alichosema ni Tamko la aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli kuruhusu wananchi walime mazao katika eneo hilo alipopita Tinde akitokea Chato Januari 29,2021 baada ya mmoja wa wananchi kutoa kero ya wananchi kuharibiwa mazao yao na TANESCO kila wanapolima.
"Rais aliruhusu wananchi tulime mazao yasiyoathiri nyaya za umeme wa TANESCO,akatoa angalizo tusipande miti wala kujenga nyumba, ndivyo tulivyofanya, sasa tumelima bahati mbaya hawa TANESCO hata ile kutoa tu taarifa kwamba tusilime haikuwepo, sasa mimi umekuta mazao yapo shambani kwanini usinishitaki tu mahakamani badala ya kuharibu mazao yangu ukaacha mahindi hayo kama yalivyo..Mahakama ndiyo itaamua kama mimi nina makosa au la.",amesema Hemed akizungumza na Malunde 1 blog.
“Mimi nimelima mazao hayo kwa jeuri ya Tamko la Rais ina maana ni sharia tosha,haihitaji tena mjadala, Rais akishasema hivi inabidi umfuate na hakuna tamko lolote lililotolewa kutengua tamko la Rais, wao wamekuja tu kufyeka mazao, wameng’oa nyanya, matikiti, vitunguu, mahindi na mbogamboga ambavyo nilikuwa nalima kwa njia ya umwagiliaji”,ameongeza Hemed.
Kufuatia tukio hilo Hemed amesema amepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 5.
Tukio hilo limezua mjadala mseto mtandaoni huku Wakazi wa Tinde na watumiaji wa mitandao ya kijamii wakihoji :
"Je Hii ni halali ? Kwanini tunarudishana nyuma namna hii? Hii Tinde pata picha huyu mkulima amelima TANESCO wakiwa wamemtazama ila leo wameamua kuja kukata mimea hivi mnadhani mwananchi atawaelewaje? Haya mahindi yana athiri nini kwenye nguzo ? Kuna mimea ya tikiti nayo imekatwa madhara ya hiyo mimea 362 ya tikiti ni yapi?".
"Tunaomba mamlaka kutusaidia kwani kitendo hiki ni ukatili dhidi ya binadamu maswali hayana majibu, Je shamba hili lilimwa siku moja na kupandwa kisha mazao kukua kwa kasi? Je Mamlaka ya Tanesco haikuwahi kufika hapo tangu shamba linalimwa hadi mazao yalipochanua kiasi hicho ndipo wakayaona?...
"Na je kwa kwa kuwa yalikuwa yamelimwa na kuchanua kiasi hicho kile kinachoitwa taratibu zingine ukiacha Sheria na kanuni zilishindwa kufanyika na kuonya? au yalikuwa maksudi ya kufanywa ukatili huo ndiyo maana mahindi yakaachwa yapendeze ndipo yafyekwe? Bado tunajiuliza tukisubiri taarifa za kimamlaka", wameendelea kuhoji watumiaji wa mitandao ya kijamii walioona video clip hiyo.
Naye Mkazi wa Tinde, Azza Hilal Hamad ambaye amewahi kuwa Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga amesema :"Nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa tarehe 29/01/2021 ,siku ambayo Hayati Dkt. John Joseph Magufuli aliposimama Tinde Barabara ya Nzega kuingia TShule ya Msingi Tinde ,akitokea Kahama na Kagongwa kuzindua mradi wa maji wa ziwa Victoria akielekea Tabora kuzindua mradi wa maji wa ziwa Victoria, aliwashukuru wananchi wa Tinde kwa kumchagua kuwa Rais, kwa kuchagua Madiwani na mbunge wa CCM, baada ya kumaliza kuongea,mwananchi mmoja ( Mzee Mayunga Mayunjanda) alijitokeza akanyoosha mkono kuomba kuongea, Hayati Mhe. Magufuli alimruhusu ,mzee yule aliomba wananchi waruhusiwe kulima kwakuwa hawaweki mazao ya kudumu na wala hayafiki kwenye nguzo za umeme.
Mhe. Rais aliruhusu na kusema waachwe wananchi walime wasibugudhiwe, kikubwa hawagusi wala kuharibu miundombinu na kwa kuwa ilikuwa kipindi cha masika watu wengi walilima siyo mahindi tu,mpaka mpunga na walivuna hakuna aliyeharibiwa mazao yake leo kumetokea kitu gani? naamini Viongozi wote walikuwepo Mh RC,Mh DC,Wakurugenzi,Wabunge,Madiwani n.k.
Hata baadhi ya Waandishi wa habari walikuwepo kama agizo hilo hilo wahusika waliliheshimu na wakawaacha watu wakalima,leo watupe aliyetengua agizo hilo na kwenda kufyeka mahindi,na matikiti ya Mwananchi huyu.
Walikuwa wapi wakati analima mpaka mazao yamefikia hatua hiyo? na kama agizo limetenguliwa ni vizuri Busara ingetumika kuelimisha na siyo huo unyama uliofanyika", - Azza Hilal Hamad
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com