Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANAMKE AANZA KUTOKWA MAZIWA KWENYE KWAPA BAADA YA KUJIFUNGUA


Kujifungua mtoto kunakuja na mabadiliko mengi katika mwili, mabadiliko ambayo megine ni ya kawaida na yasiyo ya kawaida.

Mwanamke mmoja huko Ureno baada ya kujifungua akakutana na mabadiliko ya mwili ambayo yameibua maswali mengi na udadisi wa kisayansi: Alianza kutokwa na maziwa katika kwapa lake , kwa mujibu wa taarifa.

Mwanamke huyu mwenye miaka 26 amewaambia madaktari kwamba, alianza kusikia maumivu kwenye kwapa lake la kulia, siku mbili baada ya kujifungua, kwa mujibu wa jarida la utabibu la The New England, lililochapishwa Julai 29 mwaka huu.

Madaktari walipofanya uchunguzi wa eneo hilo la kwapa, wakagundua kama uvimbe wa duara mkubwa kwa ndani. 

Cha ajabu, eneo hilo "likiminywa ama kukamuliwa linatoa majimaji meupe," aliandika mwandishi aliyeandika ripoti ya mama huyo kutoka Hospitali ya Santa Maria iliyoko Lisbon, Ureno.


Akaanza kupatiwa matibabu kwenye eneo hilo yanayotambulika kitaalam kama polymastia, ama uwepo wa tishu za ziada za matiti kwenye mwili. Kwa mujibu wa jarida la Mayo Clinic, lililochapishwa mwaka 1999 asilimia 6% ya wanawake wanazaliwa na tatizo hili la kuwa na tishu aa mkusanyiko wa seli za ziada za maziwa matiti mwilini.

Wakati mwingine tishu hizi za ziada husababisha mpaka kutokea kwa chuchu kabisa ama weusi wa duara unaofanana kabisa na ule unaozunguka chuchu, lakini kuna wakati zinazoonekana ni tissue tu za matiti, bila kuwa na chuchu ama weusi unazozunguka chuchu.

Wataalam wanasemaje?

Kwa mujibu bwa wataalamu, hali hii hutokea wakati wa ukuaji wa mimba, ambapo seli za mama kwenda kwa mtoto hutengeneza kitu kama mstari wa maziwa ambao hutoka kuanzia kwapani hadi kwenye kinena, hiyo ni kwa mujibu wa jarida la Marekani la Roentgenology.

Kawaida mistari hii hupotea na kubaki ya kwenye matiti tu. Lakini isipotokea hivyo, na kusalia katika baadhi ya maeneo ya mwili, maana yake mwili huo husalia na tishu za matiti. Na sehemu ambayo mara nyingi husalia ni kwenye makwapa, hasa kwapa la kulia.


Kama tishu hizo za matiti za kuhifadhi maziwa hazitakuwa na chuchu, ni ngumu kuigundua kawaida kama ni tishu za ziada za matiti mpaka mtu alizonazo apate ujauzito au atakapoanza kunyonyesha.


Mpaka kufika wakati hu, maziwa huteremka, kupitia tishu hizo kama ilivyo kwa matiti ya kawaida ya mzazi yanayotoa maziwa. Na wenye tatizo hili, huwa na kama uvimbe na hupata maumivu makali katika eneo la kwapa.

Baadhi ya wanawake wanaweza hata kukamua maziwa ya kutosha tu kutoka kwenye tishu hizi za ziada za kwapani.

Jarida la Mayo Clinic lilichapisha taarifa ya mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 18 aliweza kukamua maziwa kwenye kwapa lake kwa wiki nane mfululizo ili kupunguza maumivu na kuendelea kunyonyesha mtoto wake.

Kwa kisa hiki cha mwanamke wa Ureno, amehakikishiwa kwamba tatizo hilo sio kubwa na la kutisha na tishu hizo haziweza kusambaa kwenda kwenye maeneo mengine ya mwili. Madaktari wamemfahamisha kuwa anapofanya uchunguzi wa kansa ya matiti anapaswa pia kufanya uchuguzi na kwapa lake, lenye tishu zinazofananana na matiti na kutoa maziwa.


Hata hivyo haijafahamika wazi kama mwanamke huyo aliweza kutumia kwapa hilo kumnyonyesha mtoto ama kukamua maziwa yake na kumpatia mtoto.

CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com