Ngoma za Wagika zikiwa katika mbina kijiji cha Mwamlapa wilayani Bariadi mkoani Simiyu hivi karibuni wakijiandaa kwa ajili ya mashindano ya mbina za kisukuma. (Picha zote na Costantine Mathias).
Mchezo wa ngoma za asili pamoja na zana mbalimbali ambazo hutumika katika mchezo wa Utamaduni kwa kabila la wasukuma (Mbina), mchezo ambao hufanyika mara baada ya mavuno kila mwaka.
Zana za kuchezea Ngoma za asili pamoja na wachezaji wa mbina wakiwa uwanjani tayari kwa kushindana, mchezo ambao hushindanishwa kutokana na wingi wa watu.
Wagalu wakiwa na ngoma zao katika mbina kijiji cha Mwamlapa wilayani Bariadi mkoani Simiyu, wakiwa tayari kuanza mashindano ya mbina. (Picha zote na Costantine Mathias).
Na Costantine Mathias - Gamboshi
Katika toleo lililopita tuliangalia kuhusu asili ya Jina Gamboshi
Leo tunaangazia kuhusu Mbina.
Kila jamii au kabila lina mila na utamaduni wake ambao uliasisiwa na viongozi wa kimila wa eneo husika kwa lengo la kuenzi tamaduni zake pia hufanya kabila hilo kujitofautisha na makabila mengine.
Aidha kila kabila hutambulika na kujitofautisha kwa mavazi, vyakula, mtindo wa maisha, shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo na ufugaji pamoja na masuala ya kuoa na kuolewa.
Kwa sasa kabila la wasukuma ambalo limesambaa katika mikoa ya kanda ya ziwa,kanda ya kati, nyanda za juu kusini pamoja na mikoa ya Ruvuma, Mtwara hadi Kigoma wakitafuta malisho na ufugaji.
Tamaduni inayolitofautisha kabila hili na makabila mengine ni mchezo maarufu wa Mbina, mchezo huu huchezwa mara baada ya shughuli za kilimo kukamilika na kwamba hushindanishwa kwa pande mbili kulingana na idadi ya watu.
Wingi wa watu katika mbina hizi hutegemea namna wananchi walivyopata mavuno ya kutosha, kwani ikitokea wakakosa mavuno mchezo huu hufanyika kwa nadra sana sababu watu hutumia muda huo kutafuta chakula kwa ajili ya familia.
Waanzilishi wa mbina Gamboshi.
Katika ukanda wa vijiji vinavyozunguka Gamboshi, majina ya Mwana Makulyu na Mwana Mabula ukiyataja yanaonekana kusadifu masuala ya kishirikina na masimulizi yake.
Majina hayo ya wakina mama hawa wawili ambao walionekana kuwa wapambanaji wa masuala ya mbina katika ukanda wa Gamboshi, vijiji vya Gambosi, Miswaki, Nyamswa, Ngulyati Ditima, Lulayu na Mwasubuya ni Mwana Makulyu na Mwana Mabula.
Katika simulizi zao, wakinamama hawa walijaliwa kuzaa mtoto mmoja mmoja kwa kila moja na kwamba walikuwa wakichuana kwenye mbina kwa kushindania madawa.
Inaelezwa kuwa Mwana Mabula alikuwa Mgalu na Mwana Makulyu alikuwa Mgika, hivyo kila mmoja alionyesha ubabe wake wakati wa mbina kutokana na wingi wafuasi aliokuwa nao.
Inadaiwa kuwa walishandana kwa kutumia madawa ya kienyeji, na zaidi kuonyesha maajabu katika mchezo huo ambao unavuta hisia za mashabiki na watazamaji huku upande mmoja ukitumia jua kushinda na upande mwingine ukitumia mvua kushinda.
Mwana makulyu na Mwana Mabula wanatajwa kuwa washindani na waanzilishi wa mchezo huo wa mila ya kabila la wasukuma sababu walivuta hisia za watu wakati huo wakiwa ni wanawake, licha ya mchezo huo kuwepo enzi na enzi.
Bahati Magamula mkazi wa Gamboshi anasema kutokana na wakina mama hao kuzaa mtoto mmoja mmoja, pia waliweza kuwatengenezea dawa za uzazi wanawake wenzao ili waweze kupata watoto.
‘’Walikuwa wana uwezo wa kutengenezea dawa wanawake wenzao (kwalika) hali hiyo iliwafanya kuwa na kundi kubwa la wateja na wafuasi…pia wakati wa mbina walikuwa na maajabu’’ anasema Magamula.
Anasema katika uzao wao wakina mama hao, Mwana makulyu alikuwa na mtoto mmoja aliyeitwa Njile na Mwana mabula alikuwa na mtoto mmoja aliyeitwa Ngolo.
Anafafanua kuwa, mchezo wa mbina hauwezi kuchezwa na mtu mmoja, hivyo wakina mama hao kila mmoja kwenye timu walialika majirani zao kwa ajili ya kuwasaidia.
‘’Kila mwalika alikuja na mbinu (mabinda) za ushindi, mbinu hizo zilionekana za akina mama hao, mfano wakati wa mbina inaweza kunyesha mvua upande wa pili, lakini upande mwingine jua linachoma, kutumiana siafu, vyura pamoja na mengineyo ili kuburudisha’’ anasema Magamula.
Anasema kwamba wakina mama hao walitengeneza maajabu kwenye mbina kukifanya kijiji hicho kufahamika kama sehemu ya wachawi, mbina nyimbo zilizokuwa zinatumika zilielezea simulizi za maajabu.
Wilson Heka anasema elimu na dini zimewapunguzia watu kuwa na imani potofu, kuabudu miungu, mbina pamoja na kupiga ramli chonganishi ambapo kwa sasa jamii imepata mwamko wa kutumia tiba za kitaalamu.
‘’Neno la Mungu limewatoa kwenye imani potofu, huduma za afya. Elimu na maji pia mahitaji ya jamii yapo katika maeneo yetu ambayo zamani yalikithiri kwa mila na desturi za mbina’’ anasema Heka.
Anaeleza kuwa huko nyuma maisha yalikuwa magumu sana, huduma za kijamii hazikuwepo kutokana na imani za kishirikina, pia ulikuwa hauishi mwezi matukio ya watu kukatwa mapanga yanaripotiwa.
Anasema elimu imeondoa mitizamo yote ya kishirikina na yeye anasoma jamii ilikuwa ikiwatazama sana lakini wamefanikiwa kupata elimu na kuweza kuondoa mtizamo hasi.
Heka anawaomba waandishi wa Habari kutembelea mara kwa mara kijiji hapo ili kuuelimisha na kuuhabarisha umma juu ya ukweli na hali halisi ya maisha na maendeleo ya wananchi kijiji hapo.
Mayala Lukas Mkazi wa Mwamlapa anasema mchezo huo ni wa enzi za mababu zao na kwamba husherehekewa na Jamii na Wasukuma kuanzia mwezi wa tano hadi wa tisa baada ya mavuno ambapo pia hukutanisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali kushuhudia burudani hiyo.
‘’Tamaduni za mbina ni za kisukuma na mbina huchezwa kila mwaka, hushindana kijadi na kijamii imeaandaliwa kiwilaya hadi kitarafa…tunamuomba Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo afike kutazama mbina hizi ili aweze kuwashika mkono’’ anasema Mayala.
Anafafanua kuwa utamaduni wa mbina hizo ukitangazwa ndani na nje ya nchi utaleta maendeleo kijamii, kiuchumi, kimichezo na kiutalii kwa sababu watu wengi hutoka maeneo mbalimbali hadi nje ya nchi hufika kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo.
Buhuru Mahodi mkazi wa kijiji cha Kilalo anasema mbina ni utamaduni wa kabila la wasukuma ambapo mchezo huo hufanyika baada ya mavuno na kwamba hutambiana kutokana na wingi wa watu.
Subi Bunzali kutoka kijiji cha Sakwe anaiomba serikali kuonyesha ufadhili kama wanavyofanya katika michezo mingine nchini ili kuweza kuutambua mchezo huo pamoja na wachezaji.
Leah Mahuma mkazi wa Nyamswa anasema ngoma za asili (mbina) kuchezwa katika maeneo yao kila mwaka kwa amani, furaha na ushindani ambapo utamaduni huo huenzi mila na desturi za kale za jamii ya wasukuma.
Anaiomba serikali kuongeza hamasa katika mchezo huo sababu hauna madhara yoyote kijamii bali umejikita kudumisha mila za wasukuma ambapo imekuwa sehemu ya kujipatia vipato kwa Mamanju.
Hata hivyo mchezo wa Mbina umekuwa maarufu katika ukanda huu wa jamii ya kabila la wasukuma baada ya mavuno, pia imekuwa sehemu ya vijana wa kike na wa kiume kupata wake au waume.
Inaelezwa kuwa kupitia Mbina wanawake na waume huoa au kuolewa (kwa kutoroshana) pindi wanapokuwa wameenda katika kutazama mchezo huo wa asili.
Soma pia: