Na Farida Saidy Morogoro
Maofisa kutoka idara ya ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero wamenusurika kifo baada ya baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Melela kata ya Chita halmashauri ya Wilaya ya Mlimba kushambulia gari la mkurugenzi wa hamalshauri hiyo walilokuwa wakitumia na kulichoma moto pamoja na pikipiki.
Inadaiwa wananchi hao walichukua uamuzi huo baada maofisa hao kufika kwenye shamba la mwekezaji ambaye anadaiwa kwa muda mrefu hajaliendeleza shamba hilo, inadaiwa wananchi walivamia shamba hilo na kuanza kuishi zaidi ya miaka 20 sasa.
Maofisa hao walipofika walitaka kufanya upimaji ndipo wakavamiwa na gari kuwashambulia na kuchomwa moto.
Kufuatia tukio hilo, watu sita wanashikiliwa na jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kuchoma moto mali mbalimbali za serikali ikiwemo gari aina ya Land Cruiser ,pikipiki tatu,kifaa cha kupimia mipaka ya mashamba na kompyuta mpakato 3.
Akizungumza na waandishia wa habari ofisini kwake kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Fortunatus Musilim amesema tukio hilo limetokea katika kijiji cha Melela kata ya Chita Wilaya ya Kilombero,ambapo watuhumiwa walitenda kosa hilo baada ya maofisa wa Ardhi kufika katika shamba linalomilikiwa na marehemu Daud Balali ambaye alikuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Aidha Musilim ameongeza kuwa katika tukio hilo dereva aliyefahamika kwa jina la Damas Sanga (51 ) alijeruhiwa baada ya wananchi hao kumkukuta kwenye gari na kuanza kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kwa upande wake Kamishina msaidizi wa Ardhi mkoa wa Morogoro Frank Minzikuntwe amesema vurugu hizo zimetokea baada ya maamuzi ya serikali ya kulipima shamba hilo ili liweze kupangwa upya matumizi yake baada ya kutelekezwa kwa muda mrefu huku wananchi wanalolizunguuka wakikosa maeeneo ya kulima.
Social Plugin