Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewatwisha mzigo wa mambo makuu matano viongozi wa dini wa Kanisa Anglikana kwa kuwataka kutimiza wajibu wao kwa jamii katika masuala ya maendeleo na kuacha alama ya utumishi wao.
Miongoni mwa mambo hayo matano ni kuhamasisha wananchi kukubali kuchanjwa chanjo ya Ugonjwa wa Corona, kusuluhisha migogoro ya ardhi,kujiunga na mifuko ya bima ya afya pamoja na kuhimiza masuala ya kilimo.
Mtaka ametoa ushauri huo hivi karibuni katika Mkutano Mkuu wa Sinodi ,Kanisa Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika uliofanyika katika Kanisa la Anglikana Mlimwa jijini Dodoma.
Akifafanua hayo Mtaka amewataka viongozi hao wa dini kuwashauri waumini wao kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Corona ambayo imezinduliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesemà wao kama viongozi wa dini ni wajibu wao kuhamasisha masuala ya afya kwa jamii ili Kuondoa dhana ya udanganyifu uliopo ambao lengo lake ni kukwamisha zoezi hilo.
Amesema kuwa kwa viongozi na waumini watakaojitokeza kwenda kuchanjwa ofisi yake itawaandalia utaratibu mzuri wa kupata chanjo hiyo bila matatizo.
"Niwatoe hofu kuwa chanjo hiyo ni salama na ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassani ameizindua kwa kuanza kuchanjwa yeye,suala la uhai wa mtu ni mtu mwenyewe, mtu si mali ya kanisa wala serikali ukifa anaondoka mwenyewe duniani analiacha kanisa na nchi,"amesemà Mtaka.
Pamoja na mambo mengine Mtaka, amewahamasisha viongozi na waumini wao kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kupata unafuu wa matibabu pindi wanapopata udhaifu wa kiafya.
Aidha ametumia nafasi hiyo pia kueleza makakati wake wa kuinua zao la alizeti ikiwa ni Pamoja na umuhimu wa kuijakinisha Dodoma kwa kutoa wito kwa kila kiongozi na muumini kupanda miti ya kivuli na matunda katika makazi yao.
"Viongozi wa dini mnasimama mahali popote,nawaomba muisaidie Serikali kumasisha jamii kuachana na migogoro ya ardhi na badala yake kujikita kuendelea na juhudi za kujiletea maendeleo,"amesemà .
Kutokana na hayo ,Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Dickson Chilongani amemhakikishia mkuu huyo wa Mkoa kuwa watahakikisha wanasimamia yote aliyowaagiza .
Amesema ,ili jamii iwe na amani Kama ambayo wao husimamia neno hilo,lazima Viongozi wa dini wakubali kushirikiana na Serikali ikiwa ni pamoja na kufuata Sheria za nchi.
Social Plugin