David Nkulila enzi za uhai wake
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Mathew Nkulila (57) ambaye ni Diwani kata ya Ndembezi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatatu Agosti 23,2021 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutokana na maradhi ya moyo yaliyokuwa yanamsumbua.
Nkulila amekuwa Diwani wa kata ya Ndembezi tangu mwaka 2010 na Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mwaka 2010-2015.
Nkulila alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Novemba 24 Mwaka 2020 na ametumikia nafasi ya Meya kwa kipindi cha miezi 10 hadi umauti ulipomkuta.
David Mathew Nkulila alikuwa na maono ya kuifanya Manispaa ya Shinyanga kuwa Jiji.
Nkulila atakumbukwa kwa misimamo yake thabiti katika kutetea wanyonge, asiyekubali kuyumbishwa na kupiga vita rushwa na ufisadi.
Msiba upo nyumbani kwake mtaa wa Mabambasi kata ya Ndembezi jirani na Kanisa la Moravian.
Mazishi ya Mwili wa David Nkulila yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano Agosti 25,2021 katika makaburi ya Dodoma Ndembezi Mjini Shinyanga
Soma pia
Historia fupi ya Marehemu David Nkulila
David Mathew Nkulila alizaliwa tarehe 16/04/1964, Tabora mjini, mkoa wa Tabora.
David Mathew Nkulila alianza darasa la kwanza katika shule ya Msingi Bunda mwaka 1974, na baadae Shule ya Msingi Mkendo mwaka 1975, alihamia Shule ya Msingi Old Shinyanga mwaka 1976 na baadaye Shule ya Msingi Mwenge-Shinyanga mwaka 1977 hadi alipohitimu darasa la saba mwaka 1980 katika shule hiyo.
Baba yake mzazi na Marehemu Nkulila alikuwa mtumishi wa serikali hali iliyopelekea Marehemu Nkulila kuhama Shule moja kwenda nyingine ili kumfuata baba yake sehemu alipohamishiwa.
Marehemu David Mathew Nkulila alipata elimu yake ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Kilimo Kilosa (Kilosa Agricultural Secondary School) kati ya mwaka 1981-1984. Shule hii ya Sekondari ya Kilimo Kilosa ni maarufu hapa nchini kwa kauli mbiu yake ya "Elimu na Kazi"
Baada ya kuhitimu kidato cha nne Marehemu Nkulila alijiajiri na kazi ya Kilimo ambayo ndiyo ilikuwa kazi yake ya msingi hadi mauti yalipomkuta leo 23/08/2021.
Historia yake ndani ya Chama Cha Mapinduzi na majukumu ya kisiasa
Marehemu David Mathew Nkulila ana uzoefu wa kutosha katika masuala ya siasa. Marehemu Nkulila alijiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM) mwaka 1995. Ndani ya CCM Marehemu Nkulila amewahi kushika nyadhifa mbalimbali.
⏩ Marehemh Nkulila amewahi kuwa mjumbe wa Kamati ya Siasa ya wilaya ya Shinyanga Mjini kati ya mwaka 2013-2017
⏩ Katibu wa CCM Kata ya Ndembezi kati ya mwaka 2007-2012.
⏩ Katibu wa CCM Kata ya Ngokolo.
⏩ Katibu wa CCM Tawi la Bugoyi kati ya mwaka 2003-2007.
Nafasi alizozitumikia
⏩ Marehemu Nkulila amekuwa diwani wa Kata ya Ndembezi kwa vipindi vitatu mfululizo toka mwaka 2010 hadi leo tarehe 23/08/2021 mauti yalipomkuta.
⏩ Marehemu Nkulila amekuwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kati ya mwaka 2013-2015.
⏩ Marehemu Nkulila amekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabambasi kati ya 2004 - 2019.
⏩ 2000-2003 Mwenyekiti wa kamati ya WES mtaa wa Mabambasi.
⏩ Amekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) kwa zaidi ya miaka 10.
Kazi alizozifanya akiwa Diwani wa Kata ya Ndembezi
Marehemu David Mathew Nkulila kwa kipindi chake chote akiwa kama diwani wa Kata ya Ndembezi alifanikiwa kuwawakilisha vema kwa uadilifu mkubwa wakazi wa Kata ya Ndembezi.
(a)Alisimamia upimaji wa ardhi (viwanja) katika Mitaa ya Ndembezi na Butengwa. Awali mitaa hii ilikuwa na hadhi ya vijiji na ardhi ilikuwa haijapimwa.
(b) Alisimamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika viwango vya lami na changarawe ikiwemo mitaro, makalvati, vivuko na madaraja.
(c) Alisimamia ujenzi wa machinjio ya kisasa yaliyopo katika mtaa wa Butengwa.
(d)Alisimamia ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Ndembezi iliyopo katika mtaa wa Butengwa. Kwa sasa ujenzi huo upo katika hatua ya boma. Eneo hili la ujenzi wa Zahanati lilipatikana kufuatia juhudi zake akishirikiana na ofisi ya Mtendaji wa kata ya Ndembezi.
(e) Alisimamia utolewaji wa mikopo ya bila riba inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kutoka 10% ya mapato yake ya ndani kwa makundi ya vijana, wanawake na walemavu.
Mambo aliyoyapenda (Hobby)
Marehemu Nkulila alipenda kusoma vitabu, majarida na magazeti, Mitandao ya Kijamii na alipenda sana kuendesha baiskeli.
Soma pia:
R.I.P David Nkulila.
Social Plugin