MAZISHI YA DAVID NKULILA KUFANYIKA KESHO KUTWA JUMATANO MJINI SHINYANGA


David Nkulila enzi za uhai wake
Mazishi ya Mwili wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga David Mathew Nkulila (57) ambaye ni Diwani kata ya Ndembezi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano Agosti 25,2021 katika Makaburi ya Dodoma Ndembezi Mjini Shinyanga.

Msemaji wa familia Mary Joseph amesema kifo cha mpendwa wao kimetokea usiku wa kuamkia leo Jumatatu Agosti 23,2021 majira ya saa 11 alfajiri.

Amesema marehemu mjomba wake, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la ugonjwa wa Moyo kwa muda mrefu, ambapo alikuwa akilazwa mara kwa mara hospitalini kupatiwa matibabu na kuruhusiwa, lakini siku za hivi karibuni hali yake ilianza kuwa mbaya zaidi na hatimaye kufariki dunia.

“Marehemu ni Mjomba wangu, na kifo chake ni pigo kubwa katika familia yetu, amefariki kwa ugonjwa wa Moyo, ameacha watoto wanne, na mazishi yake yatafanyika siku ya Jumatano Mjini Shinyanga katika Makaburi ya Dodoma yaliyopo kata ya Ndembezi ”amesema Mary.

Nkulila amekuwa Diwani wa kata ya Ndembezi tangu mwaka 2010 na Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mwaka 2010-2015.

Nkulila alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Novemba 24 Mwaka 2020 na ametumikia nafasi ya Meya kwa kipindi cha miezi 10 hadi umauti ulipomkuta.

David Mathew Nkulila alikuwa na maono ya kuifanya Manispaa ya Shinyanga kuwa Jiji.

Nkulila atakumbukwa kwa misimamo yake thabiti katika kutetea wanyonge, asiyekubali kuyumbishwa na kupiga vita rushwa na ufisadi.

Msiba upo nyumbani kwake mtaa wa Mabambasi kata ya Ndembezi jirani na Kanisa la Moravian.


Soma pia


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post