Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Kenani Kihongosi akizungumza na waandishi wa habari leo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Kenani Kihongosi akizungumza na waandishi wa habari leo
Na Dotto Kwilasa, Dodoma.
JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) imetolea ufafanuzi wa safari anazofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa zinalenga kuimarisha mahusiano ya kimataifa na si vinginevyo.
Hatua hii imekuja wakati ambapo Rais Samia tayari amewasili nchini Zambia kuhudhiria kuapishwa kwa Rais Mteule wa nchi hiyo Hakainde Hichilema huku akifuatana na viongozi mbalimbali .
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Kenani Kihongosi amesema hayo Jijini Dodoma wakati akiongea na Waandishi wa habari huku akisisitiza kuwa Tanzania kama nchi lazima iimarishe mahusiano ya kiuchumi kwa kushirikiana na nchi nyingine.
Amesema ziara anazofanya Rais Samia Katika nchi mbalimbali zitasaidia kuondosha migogoro,kujenga urafiki kati ya nchi na nchi kudumisha amani na kufungua fursa mbalimbali.
"Fursa nyingi za kiuchumi,amani na ushirikiano tulionao na nchi nyingine vinatokana na mahusiano mazuri yaliyopo ,kupitia ziara anazofanya Mama Samia itasaidia kuondoa migogoro isiyo ya lazima,"amesema.
Katika hatua nyingine Kihongosi ametoa wito kwa vijana kuendeleza amani,mshikamano na nidhamu pamoja na kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi wa nchi na kuondokana na utegemezi.
"Nidhamu ni mali,uadilifu unapokosa nidhamu hakuna amani,na mtu yeyote anayekosa nidhamu kwa taifa lake hiyo ni msaliti,"amesema Katibu huyo wa UVCCM.