Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAAGIZA WIZARA KUFANYA MAPITIO YA SERA ZAKE


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Na Dotto Kwilasa, Dodoma

SERIKALI  imeziagiza  Wizara zote nchini zenye sera za muda mrefu kuzifanyia mapitio na kuandaa taarifa ya Utekelezaji wake kwa kuziwekea mkataba na muda  ili kuendana na mazingira ya sasa.

 Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri mkuu (Sera ,Bunge, Kazi, Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu) Jenister Mhagama wakati akizindua  mfumo wa kielektroniki wa uratibu na ufuatiliaji  wa shughuli za serikali(Dashboard).

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri huyo  amesema Utekelezaji huo wa mapitio ya sera utaongeza ari ya uwajibikaji ikiwa ni Pamoja na kuisaidia serikali katika uratibu wa shughuli zote kwa njia ya utendaji na upokeaji wa taarifa sahihi ,kwa wakati sahihi katika sekta zote nchini.

Pamoja na hayo amesema kupitia Mfumo huo wa kielekroniki shughuli za Serikali zitafanyika na kuratibiwa kwa weledi hali itakayochochea Maendeleo kwa kiasi kikubwa.

"Niwaombe watendaji wote  wa serikali  nchini kuwajibika ipasavyo katika majukumu yenu  kwa kuwa mfumo huo utakwenda kubaini utekelezaji wa shughuli zote za serikali katika kila sekta, ni lazima kila mmoja ahakikishe anasimamia majukumu yake ipasavyo,"amesisitiza.

Naye Waziri wa mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Faustine Ndugulile ambae alihudhuria uzinduzi huo amesema kuwa mfumo huo ni muhimu kwa  Wizara yake kwa kuwa unakwenda kutimiza sera ya TEHAMA nchini na  kuongeza uwajibikaji,ufanisi na uwazi kwa watumishi.

"Tunatarajia mfumo huu utarahisisha shughuli zote za kiserikali na uongeza ufanishi kwa watendaji wote katika sekta mbalimbali nchini,"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com