Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TIC NA ZIPA WASAINI MKATABA WA MAKUBALIANO KUKUZA UWEKEZAJI

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dkt. Maduhu I. Kazi( Kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Bw. Shariff Ali Shariff (kushoto) wamesaini mkataba wa makubaliano (MoU) leo  tarehe 19 Agosti, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TIC Dar es Salaam.

***

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dkt. Maduhu I. Kazi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Bw. Shariff Ali Shariff wamesaini mkataba wa makubaliano (MoU) leo tarehe 19 Agosti, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TIC Dar es Salaam. 

Lengo la makubaliano hayo ni kuhakikisha TIC na ZIPA wanashirikiana katika maswala mbalimbali ya kukuza uwekezaji Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es salaam baada ya kutiliana saini, Mkurugenzi Mtendaji wa  kituo hicho Dkt. Maduhu Kazi amesema malengo ya makubaliano hayo ni kukuza sekta ya uwekezaji upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, Dkt. Kazi amesema maeneo ambayo yamepewa msukumo mkubwa katika mashauriano hayo ni pamoja na kufanya utafiti vyanzo vya uwekezaji pamoja na kubadilishana taarifa, uzoefu na ujuzi kwa wafanyakazi wa taasisi hizo.

Maeneo mengine ni kutangaza vivutio vya uwekezaji kwa pamoja, pia kushirikiana kwenye maonyesho yanayohusu masuala ya uwekezaji huku akisisitiza kwamba masuala ya kimifumo (tehama) kuhusisha pande zote mbili (Tanzania Bara na Zanzibar) tayari wataalamu wameanza kuyafanyia kazi.

"Tutashirikiana vizuri na ZIPA katika maeneo mbalimbali, mfano masuala yakutangaza vivutio vya uwekezaji pamoja na kuandaa kwa pamoja maonyesho ya uwekezaji, kufanya tafiti mbalimbali za kutangaza na kuvutia  wawekezaji, lakini eneo jingine muhimu ni kubadilishana uzoefu na ujuzi kwa watumishi wetu",alisema Dkt. Kazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na TIC inaonyesha kuwa hali ya uwekezaji nchini  Tanzania inazidi kupanda na kushika nafasi ya kwanza kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki  licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa Uviko 19, hivyo kufuatia hali hiyo mashirikiano hayo ya ZIPA na TIC yataongeza zaidi idadi ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukuzaji Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Shariff Shariff amesema kwamba kupitia mashirikiano hayo yatasaidia kupiga hatua kubwa yakutangaza vivutio vya uwekezaji ili kukuza sekta hiyo.

" Mashirikiano haya yanaleta mafanikio makubwa sana, hivyo ZIPA na TIC tutahakikisha tunafanya kazi hizi kwa pamoja ili kufikia malengo yetu”, alisema Shariff.

"Kinachonifurahisha zaidi haya mashirikiano yamebarikiwa na wakuu wa nchi, tutashirikiana vizuri katika kutekeleza mambo muhimu yakukuza sekta ya uwekezaji kwa kutangaza vivutio vya uwekezaji vya Tanzania bara na Visiwani Zanzibar" aliongeza.

Makubaliano hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa TIC mtaa wa Shaaban Robert, Dar es Salaam tarehe 19 Agosti, 2021.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com