Livingstone Lusinde maarufu kama Kibajaji
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM -Taifa (MNEC) na mbunge wa jimbo la Mvumi mkoani Dodoma Mh. Livingstone Lusinde maarufu kama Kibajaji amewakingia kifua wabunge wenzake na kutaka wasilaumiwe kuhusu tozo za makato ya simu kwa madai kuwa wao ndiyo chanzo na kusema kuwa wanaolalamika wanapaswa kuheshimu Sheria za nchi.
Hatua hii imekuja kufuatia kuwepo kwa malalamiko kuwa Sheria hiyo ya tozo imeanzishwa na Wabunge kutokana na kile kinachodaiwa kuwa wao haiwaumizi kwa kuwa hawana makato yoyote na hawalipi Kodi jambo ambalo Mbunge huyo amelipinga.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma, Lusinde ametolea ufafanuzi suala hilo na kusema kuwa walichofanya wabunge ni kupitisha sheria hiyo ili nchi iweze kujengwa kwa kodi lakini mwenye majukumu ya kuweka viwango ni Waziri husika yaani Waziri mwenye dhamana ya Fedha nchini.
Akitilia mkazo suala hilo ameweka bayana kuhusu mshahara wake kuwa ni kiasi cha Shilingi Ml.4.6 huku makato yake yanayoelekezwa kwenye kodi ya Serikali ni Sh. Ml 1.2 huku akisema kuwa wajibu wa kila mtanzania ni kulipa Kodi.
"Sisi kama wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunakatwa kodi ambazo zinaenda kwenye shughuli za kimaendeleo hapa nchini hivyo jamii iondokane na maneno ya watu kutokusema kuwa wabunge hawakatwi kodi,Jamii iunge mkono shughuli zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,"amesisitiza.
Sambamba na hayo amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa nchini kwa manufaa ya watanzania hivyo kuwaomba wabunge kusimamia fedha walizopewa za kujenga barabara katika Majimbo yao ambayo fedha hizo zimeelekezwa kwa wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA) kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Aidha Mh. Lusinde ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kukataa kudanganywa na maneno ya Mitandao ya kijamii kuhusu chanjo ya Uviko 19 ambayo imeanza kutolewa hapa nchini.
"Kubalini kuchanjwa kulinda afya,chanjo hii imeletwa kwa manufaa na sio kumuumiza mtu,"amesema.
Social Plugin