CCM YACHARUKA GAZETI LA CHAMA TAWALA 'UHURU' KUMWANDIKA VIBAYA RAIS SAMIA... YALIFUNGIA NA KUTUMBUA VIGOGO WAKE


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo.

Na Magreth Katengu na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Chama cha Mapinduzi kimesimamisha uchapishaji wa gazeti lake la Uhuru kwa muda wa siku saba  huku kikimuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuandikwa vibaya na gazeti la Uhuru ambalo ni Gazeti Chama Tawala nchini Tanzania (CCM).

Uamuzi huo umetangazwa leo Jumatano Agosti 11,2021 na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba Jijini Dar es Salaam  ambapo amesema uamuzi huo umetolewa na bodi ambayo imeenda mbali na kuunda kamati ya kuchunguza sababu za jambo hilo kutokea.

Gazeti hilo la CCM toleo la leo Agosti 11,2021 limeandika habari yenye kichwa cha habari kisemacho “Sina wazo kuwania urais 2025-Samia”, ambayo imepewa uzito mkubwa katika Ukurasa wa mbele.


"Ukifuatilia mahojiano aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan hakuna mahali alipozungumza maneno yaliyoandikwa kwenye kichwa cha habari cha gazeti la Uhuru la leo, amelishwa maneno na uungwana ni vitendo tunamuomba radhi Rais. Tunamuomba radhi Rais kwa kumlisha maneno, ukifuatilia mahojiano yoyote BBC hakuna sehemu amezungumza na muungwana ni vitendo",amesema. 

Mbali na Chongolo kutangaza kusimamisha uchapwaji wa gazeti la Uhuru kwa siku saba kuanzia leo Jumatano kwa kuandika habari ya kupotosha juu ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pia chama hicho kimewasimamisha kazi watendaji wakuu watatu wa gazeti hilo kwa madai ya upotoshaji wa kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Viongozi waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hilo, Ernest Sungura ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mhariri Mtendaji, Athuman Mbutuka na msimamizi wa gazeti hilo Rashid Zahoro.

"Tumeamua mambo kadhaa, bodi ilikutana na kuleta taarifa ya hitimisho la kikao chao, ninaipongeza kwa uamuzi walioufanya na mimi kama Katibu Mkuu nimesimamisha kuanzia leo uchapishaji wa gazeti la Uhuru kwa siku saba, hayo ni mamlaka yangu",amesema Chongolo.

Aidha Chongolo amesisitiza kuwa hakuna mtu yoyote aliye mkubwa zaidi ya Chama Cha Mapinduzi hivyo yeyote atakayekwenda kinyume atachukuliwa hatua stahiki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post