Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga limewataka wachimbaji wadogo wa madini wametakiwa kutumia nishati ya umeme ambayo tayari imewafikia kwenye maeneo yao badala ya kuendelea mfumo wa utumiaji mafuta ya dizeli au taa katika uzalishaji wao ambao umekuwa ukiwapa hasara.
Rai hiyo imetolewa na Ofisa Mahusiano na Huduma kwa Wateja kutoka TANESCO wilaya ya Kahama Jimmy Monyo jana wakati akitoa elimu kwa wananchi juu ya usalama na matumizi bora ya nishati ya umeme kwenye Maonesho ya Wajasiriamali yaliyofanyika Mjini Kahama.
Monyo amesema nishati ya umeme tayari imesogea maeneo ya migodi midogo na wataalamu wapo wanaowafundisha wachimbaji wadogo kuacha kuendelea kutumia mfumo wa zamani wa mafuta ya taa au dizeli katika uzalishaji wao wa madini wa kila siku.
Monyo amesema kuwa Mradi wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu mzunguko wa pili upo kwenye hatua ya mwisho ikiwa jumla ya vijiji 137 vitapata nishati ya umeme ambapo idadi hiyo ndiyo ya vijiji havina umeme kwa wilaya ya Kahama.
“Sasa hivi kuna mradi wa uzalishaji unaoendelea katika vitongoji 29 wilayani Kahama na maeneo ya migodi midogo iliyopata nishati ya umeme ambayo ilikuwa kilio chao kikubwa ni Mgodi wa Mwime, Mwabomba,Segese na sasa fundi wanaendelea na ufungaji kwenye mgodi wa Nyangarata ambapo wako kwenye hatua za mwisho”, ameeleza Monyo.
Monyo amewataka wananchi kuendelea kutuma maombi ya kuunganishiwa nishati ya umeme kwa gharama ya sh 27,000 kwenye maeneo yote ya mijini na vijijini.