Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Imeelezwa kuwa gharama kubwa za vifurushi vya Intaneti na tozo mbalimbali zilizoanzishwa na serikali vinakwamisha Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano nchini na kusababisha vijana kukosa ajira na kuzorotesha biashara mtandaoni.
Hayo yamesemwa leo Agosti 11,2021 na Joel Mwankina Ntile kutoka taasisi ya Chanzo Initiative wakati mkutano wa kujadili mafanikio na changamoto za kutumia Mtandao Tanzania, uliofanyika katika Mtandao wa Zoom ukienda sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kupitia Mradi wa Boresha Habari unaoendeshwa chini ya uratibu wa mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Internews na FHI 360 unaofadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Ntile amesema Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano yamefungua ajira kwa vijana kwa kuanzisha youtube channel na website. Pia yameondoa ukiritimba kwenye vyombo vya habari na imerahisha biashara kwa njia ya mtandao, huduma za simu na Kibenki hivyo kuwezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana.
"Kutokana na maendeleo haya hivi sasa Mawakala wa Kibenki wapo zaidi ya 40,000 , Mawakala zaidi ya Laki moja na nusu wanatoa huduma za kifedha Tanzania",amesema Ntile.
"Kutokana na hali hii ni vyema sheria zetu ziwe msaada kwa wananchi ili waweze kupata ajira. Eneo la Teknolojia ya habari na mawasiliano liangaliwe vizuri",ameongeza.
Amezitaja baadhi ya changamoto zilizopo kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano ni pamoja na ada na tozo mbalimbali zilizoanzishwa na serikali zimeporosha idadi ya watumiaji wa Intaneti lakini pia gharama kubwa za vifurushi/Bando kufikia mawasiliano kwani gharama zimekuwa kubwa hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kufikia mawasiliano.
"Serikali ingeweka utaratibu wa kulinda usalama na kanuni za tozo
Serikali ingejikita kuchukua kodi kwa makampuni makubwa kama Youtube na Netflix badala ya kuwabana na vijana hawa wadogo",ameeleza Ntile.
Katika hatua nyingine amesema bado wanaaachwa nyuma kwenye maendeleo ya teknolojia na mawasiliano katika matumizi ya Teknolojia ya habari na Mawasiliano akieleza kuwa ni Asilimia 34 tu ya wanawake barani Afrika wanamiliki Smartphone hususani wale wanapatikana mjini.
Aidha amesema upo umuhimu wa kulinda watoto mtandaoni akibainisha kuwa ili kuwasaidia watoto dhidi ya madhara ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni lazima wapewe elimu ya mawasiliano.
"Upo umuhimu pia kwa wadau waungane na kuangalia namna ya kuoanisha suala la teknolojia ya habari na mawasiliano kwa watoto ili watoto waje wawe wafanyakazi wazuri na watumiaji wazuri wa mitandao ya kijamii",ameeleza.
"Huu ni muda muafaka wa kuingiza suala la mitaala ya elimu ioanishe na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili watoto waje watumie mitandao na kutumia ajira zinazopatikana mtandaoni kwa ajili ya kusaidia jamii yao, kusaidia ajira vijana wenzao na kujipatia kipato",ameongeza.
Hali kadhalika amesema upo umuhimu wa kusaidia vijana wa Kitanzania mfano Tunzaa wanaoanzisha Programu za kusaidia wananchi katika sekta mbalimbali wasaidiwe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ICT, Mulembwa Mnaku kutoka Wizara ya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari amesema maendeleo ya sasa ya vijana yanategemea Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kwamba kuna fursa nyingi mtandaoni lakini bado changamoto kubwa kwa vijana ni upatikanaji wa taarifa sahihi mtandaoni hivyo ni vyema wawe makini kutafuta taarifa sahihi mtandaoni.
“Vijana wakitumia vizuri fursa ya upatikanaji wa taarifa wapata mitaji. Ni vyema Vijana wawe pamoja kwa kutengeneza forums/clubs vyuoni. Shuleni za kujadili masuala mbalimbali na fursa mbalimbali ili kusukuma ajenda zao. Vijana wanatakiwa kuwa wabunifu Mtandaoni”,amesema.
Munakua amesisitiza Vijana wapate taarifa sahihi ili kupata fursa zinazolewa mtandaoni huku akiwakumbusha Wazazi kuwa wanayo nafasi kuhakikisha wanalea vijana wao vizuri kwani malezi ya sasa na ya zamani ni tofauti.
Kuhusu suala la Tozo za Simu, Munaku amesema tayari Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu ameagiza suala la tozo za simu liangaliwe upya, lifanyiwe kazi hivyo litatolewa mwelekeo mpya na sheria zitafanywa kuwa wezeshi kwa vijana.
"Napenda kuwataarifu pia kuwa Shirika la Posta Tanzania limeanzisha huduma ya biashara mtandaoni kupitia https:// www.postashoptz.post/ . Hii ni fursa kwa vijana kufanya biashara kupitia mtandao huu au mitandao mingine ambapo mtu anapelekewa bidhaa popote alipo",ameongeza Munaku.
Naye Shaban Maganga kutoka Internews amewataka vijana kutumia mitandao kupata fursa badala ya kufuatilia mambo yasiyo na tija
"Vijana tumieni Data vifurushi vyenu kwa ajili ya kutafuta mambo yenye tija badala ya kufuatilia umbea",amesema Maganga.
Nao washiriki wa mkutano hao kutoka mikoa mbalimbali nchini wameiomba serikali kupunguza gharama za virufurushi na kuomba lichukuliwe kwa namna ya pekee ili kuwawezesha watumiaji wa mitandao kufikia mitandao ya kijamii ili kutafuta fursa mbalimbali huku wakiomba suala la tozo za simu lifanyiwe kazi haraka.