Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WANANCHIIIIIIII Young Africans SC wamedhamiria kufanya makubwa msimu ujao baada ya kuwashusha Wakongo wengine wawili katika Kikosi chao ambao ni Beki wa pembeni (Full Back Right), Djuma Shaaban na Winga teleza, Jésus Ducapel Moloko waliotua leo kutokea nchini DR Congo.
Yanga SC wamekamilisha usajili wa Wachezaji hao kutoka AS Vita Club ya DR Congo awali walianza na Djuma Shaaban, wakafuata Heritier Makambo na Fiston Mayele huku Moloko akitajwa kuwa mrithi wa Tuisila Kisinda aliyetua Morocco katika Klabu ya RS Berkane.
Akizungumza na Azam TV baada ya kuwapokea Wachezaji hao, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga SC, Haji Mfikirwa amesema Wachezaji wote wataingia katika kambi ya timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao kwa kambi ambayo itakuwa nchini Morocco.
“Walisema Djuma hafiki, yuko wapi? sasa huyu hapa kashafika tayari kujiunga na wenzake katika kambi ya maandalizi ya msimu nchini Morocco, tunawashukuru sana GSM kufanikisha kushawishi Wachezaji hawa na kuwaleta nchini kuitumikia Yanga SC”, amesema Mfikirwa.
Mchezaji Djuma Shaaban amesema amesaini miaka miwili Yanga SC kwa lengo moja tu kuipandisha timu juu na kutwaa Ubingwa wa Ligi msimu huu na kuifikisha mbali Yanga katika mashindano ya Kimataifa ambayo timu hiyo inashiriki.
Mrithi wa Kisinda, Jesus Moloko amesema atafanya vizuri zaidi ya Kisinda kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri katika mashindano ambayo inashiriki msimu huu unaoanza mwezi Septemba.
“Tutaoambana sana kuifanya Yanga SC kuwa juu na kuchukua Ubingwa wa Tanzania kuingia hatua ya makudi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Tuisila Kisinda namjua nimecheza naye sana na mimi nimekuja hapa nitafanya vizuri zaidi yake”, amesema Moloko.
Usajili wa Yanga SC msimu huu hadi sasa ni Makipa, Djigui Diarra, Erick Johole, mabeki Djuma Shaaban, Brayson David, wengine ni Dickson Ambundo, Fiston Mayele, Khalid Aucho, Heritier Makambo na Yusuph Athumani.