ASKOFU RUWAI’CHI : NITOE AGIZO, KILA PADRE AKACHANJWE, TUSIFANYE UTOTO, UVIKO -19 INATUONDOLEA UHAI


Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Tadheus Ruwai’chi amewaagiza mapadre wote wa jimbo hilo kupata chanjo ya ugonjwa wa Corona .

Askofu Ruwa’ichi ametoa wito huo leo Jumanne, tarehe 24 Agosti 2021, katika Kituo cha Hija cha Pugu, jijini Dar es Salaam, wakati akihubiri kwenye adhimisho la misa takatifu ya mazishi ya Padri Paul Peter Haule.

Padri Haule aliyefariki dunia tarehe 18 Agosti 2021, kwenye Hospitali ya Kardinali Rugambwa, Ukonga, akipatiwa matibabu. Alikuwa Paroko Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay mkoani Dar es Salaam.

“Tulimuomba Mungu ajaalie kupatikana kwa chanjo sasa imepatikana badala ya kutumika watu wameingia katika malumbano ya kusema haya na yale dhidi ya chanjo

“Tusingojee hadi mambo haya yatutinge, tutumie vizuri fursa alizotupa Mungu kujikinga na kujihami na kwa sababu hiyo, sijui ni mapdri wangapi ambao mmeshachanjwa, lakini leo naomba nitoe agizo, kila padre akachanjwe, kila padre akachanjwe, tusifanye utoto, tusifanye lelemama, hii uviko 19 haina mjomba na shemeji na inatuondolea uhai,” amesema Ruwai’chi

Askofu Ruwa’ichi amewaomba Watanzania wafuate ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya, kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post