Mamlaka ya Bandari Tanzania ( TPA) imeandika historia baada ya meli kubwa ya kubeba magari kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam ikiwa na magari 3,743.
Kwa mujibu wa uongozi wa TPA ni kwamba kiasi hicho cha magari ambayo yameingia kwenye bandari hiyo kuvunja rekodi kwani tangu bandari hiyo ilioanzishwa haijawahi kupokea meli iliyobeba magari mengi kiasi hicho na kwamba rekodi iliyokuwepo ilikuwa ni meli iliyokuwa na magari 2600.
Akizungumza jana Agosti 10, 2021, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania( TPA) Eric Hamisi amesema meli hiyo iliyobeba magari imewasili usiku wa kuamkia jana na sasa inaendelea kushusha magari hayo ,hivyo mbali ya kuweka rekodi ya kupokea magari mengi yakiwa kwenye meli moja, habari njema ni kwamba meli hiyo imesubiria kwa chini ya saa 20.
“Tunaomba umma wa Watanzania wafahamu bandari yetu imeandika historia kwa kupoke meli ambayo imebeba magari 3743, rekodi ambayo tulikuwa nayo ni meli iliyowahi kuleta magari 2600.Haya ni mafanikio makubwa kwa bandari na nchi yetu kwa ujumla.
” Lakini hiki mabacho tunakiona leo ni mkakati wa TPA wa kuunga mkono na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sitta iliyotokana na kuboreshwa kwa miundombibu ya bandari yetu na kununuliwa vifaa vya kupakia na kushusha mizogo,lakini pili ni kutokana na mazingira mazuri ya kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
“Chakufurahisha zaidi asilimia 65 ya magari ambayo yamekuja na meli hii yanakwenda nje ya Tanzania , hii maana yake nchi zinazotuzunguka zina imani na bandari yetu na wanaridhishwa na huduma ambazo tunazitoa,” amesema.
Aidha amesema meli hiyo ya Tranquil ACE Panama mali ya Kampuni ya Metsui ambao wana uzoefu wa zaidi ya miaka 100 imetoka moja kwa moja kutoka nchin Japani na hivyo imetumia siku 20 tu badala ya siku 30 ambazo zinatumiwa na meli nyingine kutokana na kuwa na kituo zaidi ya kimoja.
Kuhusu huduma zinazotolewa na TPA ,Hamisi amesema licha kuwepo kwa janga la Covid-19 , bandari ya Dar es Salaam imeendelea kupokea mizigo kwa wingi tofauti na nchi nyingine na hiyo inatokana na mikakati madhubuti iliyowekwa na TPA.
Amesema kwa kipindi cha Juni mwaka huu TPA imehudumia mizigo tani 1.19 na Julai mwaka huu imehudumia tani milioni 1.45 sawa na ongezeko la asimia 18 ,wakati Juni mwaka 2020 TPA imehudumia tani 938,000 na Julai mwaka 2020 wamehudumia tani 800,000.
“Kwa Juni mwaka 2020 na Juni mwaka huu utaona kuna ongezeko la asilimia 28 na kwa Julai mwaka 2020 na Julai mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 23.Haya ni mafanikio makubwa na vema tukayazungumza kwa ukubwa wake.Wanaosema bandarini huduma zimedorola sio kweli,mimi ndio Mkurugenzi Mkuu wa TPA na huu naowaambia ndio ukweli,tuko vizuri sana na utoaji huduma umeongezeka sana,”amesema Hamisi.
Ameongeza kwa Julai mwaka 2020 jumla ya meli walizohudumia ilikuwa meli 116 lakini kwa Julai mwaka huu wa 2021 meli ambazo wamezihudumia ni 136 sawa na ongezeko la asilimia 17.” Kwa hali hii tunayokwenda nayo matumaini yetu Agosti mwaka huu tutafanya vizuri zaidi, na huduma ambazo tunazitoa kwa ubora na uharaka,kampuni nyingi za meli zimevutiwa kutumia bandari yetu.”
Aidha Hamisi amesema lengo ni kuhakikisha bandari ya Dar es Salaam inakuwa lango la biashara sio tu nchini bali na mataifa mengine. “Vyombo vya habari tunataka muwambie walioko duniani wajue ufanisi ambao upo kwenye bandari yetu. Tunataka bandari yetu itumike kutoa huduma.
“Na ujio wa kampuni kubwa za meli hao watakuwa mabalozi wetu kimataifa,wanafurahia huduma zetu , na sasa nchi zote duniani wanapigia debe bandari zao na sisi lazima tuitangaze bandari yetu,”amesisitiza.
Kwa upande wake Meneja wa Meli hiyo nchini John Masawe amesema ujio wa meli hiyo ikiwa na magari 3743 ni historia ambayo imeandikwa TPA na amekuwa katika sekta hiyo kwa muda mrefu lakini ni mara ya kwanza kushusha magari kwa wakati mmoja kwani wamezoea meli nyingi zikishusha magari kati ya 300 na wakati mwingine 500 au 1000.
“Kampuni yetu tumekuwa tukijihusisha utoaji huduma hapa nchini kwa miaka 23 sasa lakini tukiri kwa sasa TPA imefanya maboresho makubwa sana ya vifaa na miuondombinu na matokeo yake ufanisi umeongezeka na kampuni kubwa za meli zinafurahia kuja kwenye bandari ya Dar es Salaam,”amesema.
Aidha amesema wafanyabiashara wengi wa magari wanavutiwa na bandari ya Dar es Salaam kwani magari yamekuwa salama na hakuna gari ambayo inaweza kutolewa ikiwa imeharibika,jinsi inavyopakiwa Japan au Singapore ndivyo itakavyotolewa
Social Plugin