Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Elimu Maalum Patandi Lucian Segesela,akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Elimu Maalum Patandi pamoja na Waandishi wa Habari waliofika shuleni hapo katika ziara ya kuangalia ujenzi wa shule hiyo iliyojengwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia leo Agosti 13,2021 jijini Arusha.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Elimu Maalum Patandi wakimsikiliza Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Elimu Maalum Patandi Lucian Segesela,wakati akitoa maelezo kuhsu ujenzi wa shule hiyo kwa Waandishi wa Habari waliofika shuleni hapo katika ziara ya kuangalia ujenzi wa shule hiyo iliyojengwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia leo Agosti 13,2021 jijini Arusha.
Mkuu wa shule ya Sekondari Elimu Maalum Patandi,Janeth Mollel,akitoa taarifa fupi ya shule hiyo kwa Waandishi wa Habari waliofika shuleni hapo katika ziara ya kuangalia ujenzi wa shule hiyo iliyojengwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia leo Agosti 13,2021 jijini Arusha.
Kaimu Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Arusha Mwalimu Kabesi Kabeyo akitoa pongezi kwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kuweza kuwajengea shule bora na ya kisasa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa Waandishi wa Habari waliofika shuleni hapo katika ziara ya kuangalia miundombinu ya shule hiyo leo Agosti 13,2021 jijini Arusha.
Mwanafunzi anayetoka Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro anayesoma kidato cha kwanza katika shule hiyo Muhidini Ligibuga,akielezea ubora pamoja na mazingira mazuri ya shule ya Sekondari Elimu Maalum Patandi,na kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kuwajengea shule nzuri.
Mwanafunzi kutoka Mkoani Kigoma anaesoma kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Elimu Maalum Patandi,Lucazia Stone,akiishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kuwajengea shule hiyo ambapo ameaahidi kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zake.
Muonekano wa shule ya Sekondari Elimu Maalum Patandi,iliyojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.
................................................................................................
Na Alex Sonna,Arumeru
WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Elimu Maalum Patandi iliyopo Wilayani Arumeru Mkoani Arusha wameishukuru Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kuwajengea shule nzuri yenye miundombinu bora na ya kisasa kwa ajili ya kujifunzia.
Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imetoa jumla ya shilingi bilioni 3.67 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo ambayo ina miundombinu bora na ya kisasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maaalum kutoka Mikoa mbalimbali nchini.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo Agosti 13,2021,waliofika shuleni hapo,Wanafunzi hao wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea shule hiyo kwani ndoto zao zitaweza kutimia.
Agnes Francis ambaye anatokea Mkoani Arusha amesema ndoto zake za kuendelea na masomo zilianza kufifia kutokana na changamoto za mazingira alizozipata wakati akisoma shule ya msingi yalimfanya kutofikiria kuendelea tena na masomo.
Amesema kwa sasa ndoto zake zinaenda kutumia kutokana na shule hiyo kuwa na miundombinu rafiki kwake kwa ajili ya kujifunzia ambapo ameishukuru Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kuwajengea shule hiyo.
“Hapa nilikuwa nasoma Tanga ndio nikahamia hapa kwani mazingira ni mazuri na kwenye ufundishaji kwa kweli wanafundisha sana wanajitahidi kadri ya uwezo wao,”amesema.
Naye, mwanafunzi kutokea Mkoani Kigoma anaesoma kidato cha kwanza katika shule hiyo Lucazia Stone,amesema anaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kwa kuwajengea shule hiyo ambapo ameaahidi kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zake.
“Naishukuru sana Serikali kwa kupitia Wizara ya Elimu kwa kutujengea shule nzuri sana ya walemavu na yenye miundombinu bora namshukuru sana Samia Suluhu Hassan(Rais wa Tanzania) kwa kutujengea shule nzuri tunaiahidi Serikali tutafanya vizuri.
“Kabla sijafika hapa nilikuwa shule ya Msingi Faraja iliyopo Mkoani Kilimanjaro shule hii inatufaa sana sisi watoto wenye ulemavu kwani ina vifaa vingi,”amesema.
Mwanafunzi huyo ametoa wito kwa wazazi kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum kwani kwa sasa kuna shule yenye miundombinu rafiki kwao.
“Natoa wito kwa wazazi waache kuwaficha watoto wao hata sisi tumepitia changamoto lakini tumekuja kufikia katika shule hii,”amesema.
Naye,Mwanafunzi anayetoka Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro anayesoma kidato cha kwanza katika shule hiyo Muhidini Ligibuga ,amesema awali ndoto yake ya kuwa mwanasheria ilianza kufifia lakini mara baada ya kufika katika shule hiyo furaha yake imeongezeka atakuja kuwatetea watanzania wanyonge baada ya ndoto yake kutimia.
“Kiukweli ndoto za kusoma nilikuwa nazo ila kabla zilitaka kukwama kabla ya kufika hapa nilipangiwa shule ya Sekondari Kilosa mwezi wa kwanza kutokana na mazingira yake ya pale siendani nayo mwalimu Mkuu akaniambia nenda nyumbani tutafanya utaratibu mwingine nimeweza kukaa nyumbani kwa muda mwingi sana.
“Lakini namshukuru mungu mlezi wangu mmoja akapata mawasiliano ya kiongozi mmoja kutoka Wizara ya elimu akaongea akanitafutia shule mpaka leo nasoma vizuri sana bila shaka yoyote.Nilipoteza kabisa matumaini ya kusoma.Kikweli wanafunzi wengine wenye mahitaji maalum wasivunjike moyo shule ipo mfano mimi ningekata tamaa nisingefika hapa,”amesema.
Mwanafunzi huyo amesema mazingira ya shule hiyo ni mazuri na mwanafunzi yoyote anaweza kusoma na kufaulu.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo,Janeth Mollel amesema shule hiyo imeanza Februari 22 mwaka huu ambapo walipangiwa wanafunzi 185 ambapo kati ya hao 136 ni watoto wenye mahitaji maalum huku 44 wakiwa ni wanafunzi wa kawaida.
Amesema shule hiyo ina Viziwi 89,walemavu wa viungo 24 ambao hawana mikono na miguu na wengine hutumia viti vya walemavu,Albinism wawili na wenye ulemavu wa kutoona wawili.
Amesema wana walimu 19 ambapo 7 ni kwa ajili ya kuwafundisha viziwi na wenye usonji ambapo amedai shule hiyo imeweza kukidhi mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Baada ya kupangiwa hawa watoto 185 watoto walioripoti ni 168 miongoni mwa wanafunzi hao 168 wale wanafunzi 136 wenye mahitaji maalum walioripoti ni 124 ina maana wanafunzi 12 hawajaripoti nimejaribu kuwafuatilia hawa watoto kwa muda mfupi niliokaa nao hawa wanafunzi wanatoka kwenye maisha magumu.
“Wengi wamekuwa wakiwakimbia tumefanya juhudi kubwa kuwapata hawa wanafunzi 124 hawa waliobaki tunaendelea kufanya jitihada kuhakikisha wanafika hapa,”amesema.
Hata hivyo,Mkuu huyo wa shule amesema wazazi wanaishukuru Serikali kwa kuwajengea shule hiyo nzuri ambapo amedai changamoto iliyopo kwa sasa ni baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kutimiza majukumu binafsi ya wanafunzi kutokana na Serikali kutoa kila kitu.
“Changamoto inayokuja kwa baadhi ya wazazi ni kushindwa kuwapatia mahitaji binafsi pamoja na kwamba Serikali inatoa kila kitu,”amesema.
Hata hivyo Mkuu huyo wa shule alimshukuru Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Joyce Ndalichako kwa kuwapatia vitabu 750 vya masomo ya Historia,Geographia na Kiingereza na viti kwa ajili ya wanafunzi walemavu.
“Naishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tarehe 17 mwezi wa tatu 2021 Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako aliwapatia wanafunzi viti mwendo vitatu,vitabu vya Historia ,Geographia na Kiigereza vitabu 750 na shule ina miezi sita tu,”amesema.
Social Plugin