Wenyeji wa kijiji cha Karando nchini Kenya wameingiwa na hofu baada ya kuamka asubuhi na kukuta jeneza lililokuwa na kuku na rozari likiwa limetupwa katika nyumba ya mmoja wao.
Wenyeji hao waliamkia kisa hicho mnamo Alhamisi, Agosti 12,2021 asubuhi. Kando na kuku aliyekuwa hai na rosari, jeneza hilo pia lilikuwa na konokono na vitu vingine vya ajabu.
Mmiliki wa boma hilo Silvestor Okero alisema waliamka asubuhi na kupata jeneza hilo likiwa limetupwa nyumbani kwake.
Okero aliingiwa na wasiwasi na kumwita mmoja wa majirani zake aje kushuhudia kile alichokiona nyumbani kwake.
"Jeneza lilikuwa limefungwa kwa hivyo sikulifungua lakini nikampigia mmoja wa majirani zangu aje kunisaidia kuhusiana na suala hilo zito," Okero alisema.
Mwanaume huyo alisema maishani mwake hajawahi kushuhudia vituko kama hivyo namkuongeza kwamba amekuwa akiishi kwa amani na watu na wala hana uadui wowote na yeyote.
"Sina tatizo lolote na mtu yeyoye lakini nashuku huenda kisa hiki kimetekelezwa na mmoja wa jamaa zangu ambaye tunazozania shamba," aliongeza.
Mmoja wa majirani zake alisema kwamba alikwenda nyumbani humo alipopigiwa simu, akaona jeneza, na kuripoti jambo hilo kwenye kituo cha polisi cha Riat; jeneza hilo baadaye lilifunguliwa.
Alidokeza kwamba wenyeji waliliondoa jeneza hilo bomani mwake na kisha wakaliteketeza na tunguri zilizokuwa ndani. Wakazi hao walishuku huenda kikawa ni kisa cha uchawi na kuwataka maafisa wa polisi kuanzisha uchunguzi.
Walilalamikia kuongezeka kwa visa vya uchawi katika eneo hilo, wakisema vimelemaza maendeleo na kuwanyima usingizi.
CHANZO - TUKO NEWS
Social Plugin