KAZI YA KUPELEKA UMEME VIJIJINI INAENDELEA – NAIBU WAZIRI BYABATO











Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato (katikati), akipiga makofi baada ya kuwasha rasmi umeme katika Ofisi ya Kijiji cha Mikere, Kata ya Njia Nne, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani. Naibu Waziri aliwasha umeme huo ikiwa ni uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili katika Mkoa wa Pwani Agosti 26, 2021. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Hadija Nasri na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.








Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mikere, Kata ya Njia Nne, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Ngazi ya Mkoa, Agosti 26, 2021.






Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwena akiwasilisha taarifa kuhusu Wakala huo, wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Pwani, uliofanyika katika kijiji cha Mikere, Kata ya Njia Nne, wilayani Mkuranga, Agosti 26 mwaka huu.






Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato (wa pili-kushoto) akishirikiana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Pwani, kukata utepe ili kuzindua rasmi Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Mkoa wa Pwani. Tukio hilo lilifanyika katika kijiji cha Mikere, wilayani Mkuranga Agosti 26, 2021. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Hadija Nasri na kushoto kwa Naibu Waziri ni Mbunge wa Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.












Wananchi wa Kijiji cha Mikere, Kata ya Njia Nne, wilayani Mkuranga, Mkoa wa Pwani, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, Ngazi ya Mkoa, uliofanyika katika kijiji hicho, Agosti 26, 2021.






*******************************








Veronica Simba na Hafsa Omar – Pwani


Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato amesema kuwa kazi ya kusambaza umeme vijijini inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi nchini kote kupitia miradi mbalimbali.


Aliyasema hayo wakati akizindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili Mkoa wa Pwani, katika Hafla iliyofanyika kijiji cha Mikere, Kata ya Njia Nne, wilayani Mkuranga Agosti 26 mwaka huu.


Akizungumza na wananchi wakati wa Hafla hiyo, Naibu Waziri alieleza kuwa uzinduzi huo ni mojawapo ya mafanikio makubwa ya Serikali kwani unakamilisha ngwe ya mwisho ya upelekaji umeme katika vijiji vilivyosalia.


Alibainisha kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni 37.431 kwa ajili ya kuvifikishia umeme vijiji vyote 89 vilivyosalia katika Mkoa wa Pwani.


Kwa upande wa Wilaya ya Mkuranga, Naibu Waziri alibainisha kuwa jumla ya shilingi bilioni 16.823 zimetengwa kwa ajili ya kuvifikishia umeme vijiji vyote 40 vilivyosalia.


Aidha, Naibu Waziri aliwahamasisha wananchi kutumia fursa hiyo adhimu ya umeme kuboresha maisha yao kwa kuutumia kwenye miradi ya uzalishaji mali pamoja na huduma mbalimbali za kijamii.


“Tunawahimiza wananchi kuanzisha viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuboresha utoaji huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano na nyinginezo,” alisisitiza.


Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwena alibainisha kuwa, Awamu hiyo ya Tatu ya Mradi, Mzunguko wa Pili itatekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara.


“Mradi huu umelenga kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji na vitongoji 3,448 na utanufaisha wateja wa awali 75,622 kwa kipindi cha miezi 18 na gharama ya shilingi trilioni 1.3,” alifafanua.


Akitoa salamu za ukaribisho, Mbunge wa Jimbo la Mkuranga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega aliipongeza Serikali kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo kwa wananchi ikiwemo miradi ya umeme vijijini.


Ulega aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Nishati na REA, kukamilisha ahadi ya kuvipelekea umeme vijiji vilivyosalia ili wakazi wake nao wanufaike na nishati hiyo muhimu.


Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili mkoani Pwani, unatekelezwa na Mkandarasi China Railway Construction Electrification Bureau Group Company Ltd (CRCEBG) na umefadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post