Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHAHIDI KESI YA SABAYA ASEMA ALIMPOKEA DIWANI BAKARI MSANGI AKIWA NA UVIMBE WA DAMU MASIKIONI NA ALAMA ZA MAJERAHA YA KUPIGWA


Daktari katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru), Ngiana Mtui (28), amepanda kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kutoa ushahidi.
Amedai  mahakamani huko kuwa alimpokea Bakari Msangi  ambaye ni Diwani wa Kata ya Sombetini akiwa na hali mbaya na alikuwa na uvimbe wa damu masikioni na alama za majeraha ya kupigwa na kitu butu.

Shahidi huyo wa 10 wa Jamhuri alipanda kizimbani jana mahakamani  kutoa ushahidi katika kesi ya jinai namba 105 yenye mashtaka matatu ya unyang'anyi wa kutumia silaha inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake wawili.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Baraka Mgaya, shahidi huyo ambaye ni mkazi wa Kata ya Baraa, Halmashauri ya Jiji la Arusha, alidai amefanya kazi ya kitabibu Mount Meru kwa muda wa miaka miwili.

Daktari huyo alidai kuwa Februari 10 mwaka huu, akiwa kazini akiendelea na majukumu yake, majira ya usiku, alimpokea mgonjwa ambaye ni Bakari Msangi, akilalamika kuwa na maumivu makali sehemu za masikio, mashavu na usoni.

Shahidi huyo alidai ngozi ya mgonjwa huyo ilikuwa ikionyesha kuumia kwa kuwa ilikuwa na rangi nyekundu na alikuwa amevimba kwenye masikio na damu ilikuwa imeivilia ndani ya sikio.

"Mgonjwa alikuwa wa jinsia ya kiume, alikuwa na mchubuko na uvimbe kwenye sehemu za usoni, mashavuni na kwenye masikio na baada ya uchunguzi, tulibaini kwamba tukio hilo lilitokea kabla ya kufika hospitalini.

"Baada ya mgonjwa kufika hospitalini na kulalamika kwamba anahisi maumivu, tulianza kumpa huduma ya kwanza na kuendelea kumpatia matibabu kwenye sehemu alizodai kwamba amepata maumivu," alidai.

Shahidi hiyo alidai kuwa baada ya kupewa huduma za matibabu kwa kipindi kifupi, Msangi alimweleza kwamba maumivu yalipungua, hivyo hawakumlaza hospitalini, lakini walimpatia dawa na akaruhusiwa kwenda nyumbani.

"Tulipofanya uchunguzi, tulibaini kwamba mgonjwa alipigwa na kitu butu ambacho kilisababisha ngozi kubadilika rangi kuwa nyekundu na damu kuivia kwenye masikio na kitu kilichotumika hakikuwa cha ncha kali au kizito kwa kuwa kingemchana au kuvunja mifupa kwenye sehemu ambayo imeshambuliwa," alidai.

Daktari huyo alidai kuwa baada ya matibabu, walijaza fomu namba tatu ya polisi (PF3) na baada ya hapo walimruhusu mgonjwa kutoka hospitalini.

"Kwa utaratibu wa kawaida baada ya mgonjwa kupatiwa matibabu na PF3, kujazwa hapewi mgonjwa bali inahifadhiwa hadi hapo askari polisi watakapokuja kuifuata na sisi tunawakabidhi wao kwa ajili ya taratibu zingine," alidai.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Mosses Mahuna, shahidi huyo alidai kwamba Februari 10, mwaka huu, hospitalini huko alikabidhiwa PF3 na ndugu wa Msangi.

Wakili Mahuna alimhoji shahidi huyo kwa nini kwenye fomu ya PF3 imejazwa na kuonyesha mgonjwa alipigwa na watu 11 wakati daktari huyo hakuwapo eneo la tukio.

Katika majibu yake, shahidi huyo, alidai kuwa baada ya kumhoji mgonjwa (Msangi) ndipo alimweleza kwamba alipigwa na watu 11, hivyo aliandika maelezo hayo kwa kuyaingiza kwenye jalada la mgonjwa.

Vilevile, Wakili Mahuna pia alimhoji daktari huyo kwa nini fomu hiyo ya FP3 inaonyesha mgonjwa huyo alipelekwa hospitalini huko Februari 10 lakini fomu hiyo imejazwa Machi 10, mwaka huu.

Shahidi huyo alidai PF3 inajazwa siku ambayo polisi wanakwenda kuichukua hospitalini kama kuna kesi na fomu hiyo haijazwi siku ambayo mgonjwa amepelekwa hospitalini.

Mbali na Ole Sabaya, washtakiwa wengine wawili katika shauri hilo ni Sylvester Nyegu (26) na Daniel Mbura (38).





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com