MKURUGENZI wa Jiji la Tanga Spora Liana akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuboresha ukusanyaji na uhifadhi wa taarifa za ardhi na maeneo ya kusaidia utoaji huduma za manispaa jijini Tanga ambapo vijana 50 kutoka Chuo Kikuu Ardhi na jiji la Tanga wamenufaika na mafunzo yaliyoanza Agosti 18 mwaka 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga kulia ni Mwakilishi wa Fondation Botnar Philotheusy Mbogoro |
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Tanzania Data Lab (dLab) Stephen Chacha akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo |
Ibrahim Msuya, Meneja wa Mradi unaotekeleza Living Lab Initiative akielezea jambo |
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia kwa umakini
MTAFITI Mkuu wa Mradi Living Lab Initiative Prof.Ally Namanganya akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo |
Katika kuboresha ukusanyaji na uhifadhi wa taarifa za ardhi na maeneo ya kusaidia utoaji huduma za manispaa jijini Tanga, wanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi na vijana wa jiji la Tanga wamenufaika na mafunzo yaliyoanza Agosti 18, 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Vijana hao 50 wanatarajiwa kujengewa uwezo wa kutumia tehama ili kukusanya taarifa za maeneo na kutengeneza mifumo taarifa za kijografia (GIS) ili kusaidia katika kuboresha huduma za ukusanyaji taka ngumu, utambuzi wa maeneo hatarishi kiafya na kiusalama, taarifa za maeneo muhimu, mitaa na majengo pamoja na mifumo ya kusimamia mipango ya maendeleo ya Jiji la Tanga.
Mafunzo hayo yatakatayofanyika kwa awamu mbalimbali kwa siku 60 ni sehemu ya Living Lab Initiative ambayo inasimamiwa na Tanzania Data Lab (dLab), Chuo Kikuu Ardhi na Halmashauri ya Jiji la Tanga ambao wamesaini makubaliano ya kufanya miradi kwa pamoja ili kutumia stadi na rasilimali za kila mmoja ili kuweza kutatua changamoto zilizopo kwenye Jiji la Tanga.
Mradi huu upo chini ya ufadhili wa Fondation Botnar ya nchini Uswis,Mradi huo unalenga kutatua matatizo ya wananchi wa Jiji la Tanga kwa kutumia takwimu na teknolojia kuwezesha wananchi na serikali kufanya maamuzi sahihi.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyokuwa ya Kiserikali ya Tanzania Data Lab (dLab) Stephen Chacha alisema wapo Tanga kuangalia miradi ya maendeleo inayotumia takwimu na ubunifu kwenye kuleta maendeleo ya jamii.
Alisema wao kama taasisi wamejikita zaidi katika kuhakikisha kuna ongezeko la matumizi ya taarifa na takwimu kwenye kufanya maamuzi na kuleta maendeleo ikiwemo kutumia ubunifu unaochochewa na matumizi ya taarifa na takwimu.
Mkurugenzi huyo alisema walianza kufanya kazi na Jiji la Tanga mwaka mmoja uliopita kwa kufanya zoezi la kuangalia kiasi gani Jiji la Tanga lilikuwa likitumia taarifa na takwimu kwenye mipango yake ya maendeleo na katika kufanya maamuzi kwenye ngazi mbalimbali.
Alisema baada ya matokeo ambayo waliyapata kwenye mchakato huo ndio waliweza kutumia msingi huo kwenye miradi wanayoitekeleza ikiwemo wa Living Lab Initiative katika kujikita kwenye kufungua fursa za data na takwimu katika Jiji la Tanga, hatua ambayo imeboresha utoaji huduma zinazotolewa na Jiji la Tanga na kuboresha maisha ya wananchi ambao wanahudumiwa kupitia serikali za mitaa.
Aidha alisema mradi huu una lengo la kuleta dhana nzima ya uchumi wa kidigitali karibu na wananchi kwani serikali inapozungumzia uchumi wa kidigitali inaelekeza nguvu zaidi katika Halmashauri na Majiji na jinsi gani wanaweza kufungua fursa ya kidigitali kupitia mifumo ya taarifa na takwimu ndani ya Halmashauri zao.
“Lengo letu ni kuwawezesha vijana ambao wengi wana changamoto ya ajira, wajue jinsi gani uchumi wa kidigitali unaweza kufungua fursa za ajira kwao kwa kuwajengea uwezo katika masuala la ubunifu na data ili kuweza kujiajiri,” alisema Chacha.
Alifafanua kwamba utekelezaji wa mradi huo unahitajika kwani sasa dunia inabadilika kwa kasi kubwa ya maendeleo ya teknolojia na mifumo ya tehama, vitu ambavyo vinaleta fursa kubwa ya kujiajiri na kuajiriwa .
“Kama tunavyofahamu, kuna vijana Tanga wameweza kupata mikataba ya kazi na mashirika ya nje, fursa za ajira na biashara. Maendeleo hayo ya sayansi na teknolojia, mifumo ya habari na mawasiliano yana mchango mkubwa sana katika hilo,” alisema Chacha.
Aidha, Meneja wa Mradi Ibrahim Msuya alisema kuwa siku tano za mwanzo zitajikita kwenye matumizi ya taarifa katika kufanya maamuzi, namna ya kuzikusanya na kuzichakata na kutengeneza teknolojia ambazo zinaweza kutatua changamoto zilizopo kwenye Jiji.
“Mradi huu ni wa miaka mitatu. Kwa sasa, tunatarajia kuanza kutatua changamoto ya ukusanyaji wa taka na wanatarajia kutoka na mfumo ambao utarahisisha ukusanyaji
wa taka,” alieleza Msuya.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Spora Liana aliwashukuru kwa kazi yao nzuri ambayo wameipanga kuifanya katika Jiji la Tanga.
Alisema kuwa matokeo ya mradi huo yatainufaisha serikali na vijana pia.
Social Plugin