Mahindi yakikatwa
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Kufuatia mijadala iliyoibuka kufuatia tukio la Wafanyakazi wa TANESCO kufyeka mazao katika shamba la Mkulima wa Tinde wilaya ya Shinyanga kwa kile kinachodaiwa kuwa amelima katika njia ya umeme, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema linafuatilia tukio hilo.
Jana usiku Alhamis Agosti 19,2021 video clip inayoonesha watu wanaodaiwa kuwa ni wafanyakazi wa TANESCO ilisambaa mtandaoni ikionesha wakikata kata mazao ya mkulima wa Tinde anayedaiwa kulima kwenye njia ya umeme.
Akizungumza na Malunde 1 blog, leo Ijumaa Agosti 20,2021 Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Narrowil Sabaya amesema kwa hatua za awali tayari amemtuma Mhandisi Mkuu wa Idara ya Usafirishaji kwenda Tinde akaonane na mmiliki wa shamba na mwenyekiti wa kijiji ajue kilichotokea ni nini hadi tukio hilo likatokea.
“Nimeona video Clip mtandaoni, nilichokifanya kwa hatua za awali, nimemtuma mhandisi Mkuu wa Idara ya Usafirishaji aende Tinde akaonane na huyo mmiliki wa shamba na mwenyekiti wa kijiji,nijue kwanza kwa hatua za awali kilichotokea ni nini mpaka tukafika huko, then from then nitajua sasa cha kusema ni kipi. nimetuma Mtu atakayeniletea taarifa sahihi. Tutatoa taarifa juu ya kilichotokea",amesema Meneja wa TANESCO mkoa wa Shinyanga.
Kwa mujibu wa mmiliki wa shamba hilo lililofyekwa mazao yake, Hemed Rashid amesema aliamua kulima mazao hayo yakiwemo Mahindi, nyanya, mbogamboga na matikiti kufuatia kile alichosema ni Tamko la aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli kuruhusu wananchi walime mazao katika eneo hilo alipopita Tinde akitokea Chato Januari 29,2021 baada ya mmoja wa wananchi kutoa kero ya wananchi kuharibiwa mazao yao na TANESCO kila wanapolima.
"Rais aliruhusu wananchi tulime mazao yasiyoathiri nyaya za umeme wa TANESCO,akatoa angalizo tusipande miti wala kujenga nyumba, ndivyo tulivyofanya, sasa tumelima bahati mbaya hawa TANESCO hata ile kutoa tu taarifa kwamba tusilime haikuwepo, sasa mimi umekuta mazao yapo shambani kwanini usinishitaki tu mahakamani badala ya kuharibu mazao yangu ukaacha mahindi hayo kama yalivyo..Mahakama ndiyo itaamua kama mimi nina makosa au la.",amesema Hemed.
“Mimi nimelima mazao hayo kwa jeuri ya Tamko la Rais ina maana ni sharia tosha,haihitaji tena mjadala, Rais akishasema hivi inabidi umfuate na hakuna tamko lolote lililotolewa kutengua tamko la Rais, wao wamekuja tu kufyeka mazao, wameng’oa nyanya, matikiti, vitunguu, mahindi na mbogamboga ambavyo nilikuwa nalima kwa njia ya umwagiliaji”,ameongeza Hemed.
Kufuatia tukio hilo Hemed amesema amepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 5.
Tukio hilo limezua mjadala mseto mtandaoni huku Wakazi wa Tinde na watumiaji wa mitandao ya kijamii wakihoji :
"Je Hii ni halali ? Kwanini tunarudishana nyuma namna hii? Hii Tinde pata picha huyu mkulima amelima TANESCO wakiwa wamemtazama ila leo wameamua kuja kukata mimea hivi mnadhani mwananchi atawaelewaje? Haya mahindi yana athiri nini kwenye nguzo ? Kuna mimea ya tikiti nayo imekatwa madhara ya hiyo mimea 362 ya tikiti ni yapi?".
"Tunaomba mamlaka kutusaidia kwani kitendo hiki ni ukatili dhidi ya binadamu maswali hayana majibu, Je shamba hili lilimwa siku moja na kupandwa kisha mazao kukua kwa kasi? Je Mamlaka ya Tanesco haikuwahi kufika hapo tangu shamba linalimwa hadi mazao yalipochanua kiasi hicho ndipo wakayaona?...
"Na je kwa kwa kuwa yalikuwa yamelimwa na kuchanua kiasi hicho kile kinachoitwa taratibu zingine ukiacha Sheria na kanuni zilishindwa kufanyika na kuonya? au yalikuwa maksudi ya kufanywa ukatili huo ndiyo maana mahindi yakaachwa yapendeze ndipo yafyekwe? Bado tunajiuliza tukisubiri taarifa za kimamlaka", wameendelea kuhoji watumiaji wa mitandao ya kijamii walioona video clip hiyo.
Naye Mkazi wa Tinde, Azza Hilal Hamad ambaye amewahi kuwa Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Shinyanga amesema :"Nakumbuka ilikuwa siku ya Ijumaa tarehe 29/01/2021 ,siku ambayo Hayati Dkt. John Joseph Magufuli aliposimama Tinde Barabara ya Nzega kuingia TShule ya Msingi Tinde ,akitokea Kahama na Kagongwa kuzindua mradi wa maji wa ziwa Victoria akielekea Tabora kuzindua mradi wa maji wa ziwa Victoria, aliwashukuru wananchi wa Tinde kwa kumchagua kuwa Rais, kwa kuchagua Madiwani na mbunge wa CCM, baada ya kumaliza kuongea,mwananchi mmoja ( Mzee Mayunga Mayunjanda) alijitokeza akanyoosha mkono kuomba kuongea, Hayati Mhe. Magufuli alimruhusu ,mzee yule aliomba wananchi waruhusiwe kulima kwakuwa hawaweki mazao ya kudumu na wala hayafiki kwenye nguzo za umeme.
Mhe. Rais aliruhusu na kusema waachwe wananchi walime wasibugudhiwe, kikubwa hawagusi wala kuharibu miundombinu na kwa kuwa ilikuwa kipindi cha masika watu wengi walilima siyo mahindi tu,mpaka mpunga na walivuna hakuna aliyeharibiwa mazao yake leo kumetokea kitu gani? naamini Viongozi wote walikuwepo Mh RC,Mh DC,Wakurugenzi,Wabunge,Madiwani n.k.
Hata baadhi ya Waandishi wa habari walikuwepo kama agizo hilo hilo wahusika waliliheshimu na wakawaacha watu wakalima,leo watupe aliyetengua agizo hilo na kwenda kufyeka mahindi,na matikiti ya Mwananchi huyu.
Walikuwa wapi wakati analima mpaka mazao yamefikia hatua hiyo? na kama agizo limetenguliwa ni vizuri Busara ingetumika kuelimisha na siyo huo unyama uliofanyika", - Azza Hilal Hamad
Soma pia :
Social Plugin