Rais mteule wa Zambia kupitia Chama cha UPND Hakainde Hichilema na Makamu wake wa Rais Mutale Nalumango
***
Mgombea wa kiti cha urais nchini Zambia kupitia chama cha upinzani cha UPND Hakainde Hichilema, ameshinda katika kinyang'anyiro hicho kwa kupata kura milioni 2.8 na kumshinda aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Edgar Lungu aliyepata kura milioni 1.8.
Hichilema amepata ushindi huo baada ya kushindwa mara tano katika chaguzi kama hizo na amemshinda mpinzani wake wa siku nyingi Edgar Lungu, ambaye amedai kwamba uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa madai ya kuwa maafisa wa chama chake waliokuwa wakisimamia uchaguzi walifukuzwa kwenye vituo vya kupigia kura.
Uongozi wa miaka sita chini ya Rais Edgar Lungu ulikosolewa kwa madai ya kukiuka haki za binadamu, ufisadi na uchumi uliodorora pamoja na ukosefu wa ajira, ambapo Rais mteule wa sasa pamoja na Makamu wake Mutale Nalumango, watakabiliwa na changamoto ya kubadilisha uchumi wa taifa hilo.
Rais mteule wa taifa hilo Hakainde Hichilema, ana umri wa miaka 59.
Uchaguzi huo umefanyika Agosti 12, mwaka huu