Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga Siriel Mchembe
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mkoani Tanga Siriel Mchembe amewaonya wanaume hususani akina baba wanaonyonya maziwa ya wake zao ambao wananyonyesha watoto kuacha mara moja kwani tabia hiyo inawafanya watoto wakose lishe kutoka kwenye maziwa ya mama.
DC Mchembe ametoa kauli hiyo maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji mara baada ya kupokea ombi kwa wanawake wanaonyonyesha wilayani Handeni kuwasaidia kupaaza sauti ili kukemea tabia hiyo inayofanywa na wanaume hao waweze kuiacha.
“Jambo la kwanza ambalo limeibuka ni wamama kulalamika kwamba wababa wananyonya maziwa na kutokana na kitendo cha wababa kunyonya maziwa kwa imani potofu kwamba yana nguvu fulani tumeona kwamba watoto wanakosa lishe kwahiyo tumekubaliana jambo hilo likemewe kwa nguvu zote,” amesema Mchembe.
"Niwashauri wale wanaume mnaonyonya maziwa ya wake zenu muache, mnatumia chakula cha watoto wenu na hiyo inasababisha mtoto kupata utapiamlo maana hapati maziwa ya kutosha, la msingi hakikisheni mnashirikiana kwenye malezi haya mambo mengine acheni," ameongeza Mchembe.
Imeelezwa kuwa wanaume hao wamekuwa na tabia ya kunyonya maziwa ya wake zao wanaonyonyesha kwa madai kuwa kwa kufanya hivyo yanaongeza nguvu za kiume huku wengine wakihusisha na imani za kishirikina.
Chanzo - EATV
Social Plugin