Na Dotto Mwaibale, Singida.
NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amekutana na wadaiwa sugu wa kodi ya pango la Ardhi Mkoa wa Singida ili kutafuta njia bora za kulipa madeni hayo.
Mabula alikutana na wadaiwa hao katikati ya wiki hii baada ya kukutanishwa nao kwenye kikao chake na watumishi wa idara za ardhi na wadau mbalimbali wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani hapa.
Alisema kwenye Sheria ya ardhi kifungu cha (33) kifungu kidogo cha (3),kinasema mtu yeyote ambaye anamiliki ardhi anatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi kama sheria inavyoelekeza.
Alisema lakini kuna baadhi ya watu baada ya kupimiwa maeneo yao hujificha na hawaendi kuomba kumilikishwa ili waanze kulipa kodi.
Alisema kutokana na hali hiyo Serikali iliona iweke utaratibu kwa mtu yeyote ambaye amepimiwa eneo lake apewa siku 90 za kuomba kumilikishwa na asipofanya hivyo baada ya siku hizo atatakiwa kulipa kodi, ambapo pia ilitoa msamaha kwa waliopimiwa kipindi cha nyuma wataanza kulipa kuanzia mwaka jana sheria ilipoanzishwa.
Mabula alisema wizara imeamua kutoa nafasi hiyo kwa wadaiwa hao kabla ya kuanza utekelezaji wa sheria ili waweze kujua wajibu wao kama raia, taasisi na watu binafsi wa kulipa kodi ambapo wizara itatoa nafasi ya mwaka mmoja waweze kulipa madeni yao.
"Niwatake watumishi wa wizara hii mkaanze kusimamia sheria, kwasababu hamsimamii sheria vizuri ndio maana mchakato huu wa kulipa kodi unakuwa mgumu,nniwaombe walipa kodi lipeni kodi zenu kila mwaka mkivusha zoezi la kulipa litakuwa zito kwasababu kiwango kitaongezeka kutokana na kulimbikiza." alisema Mabula.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida Shamim Hozza akisoma taarifa ya utekelezaji wa wizara hiyo mkoani hapa alisema mkoa ulipangiwa kukusanya maduhuri yatokanayo na ardhi Sh. Bilioni moja na milioni mia tisa lakini walikusanya Sh. Bilioni moja na milioni mia mbili sawa na 66%.
Alisema moja ya changamoto zilizosababisha ofisi yake kushindwa kufikia lengo ni madeni makubwa ya Serikali na baadhi ya taasisi za dini ambazo zimekuwa na ukakasi wa kulipa madeni hayo.
Hozza alisema ili kukabiliana na changamoto hizo ofisi yake inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhamasisha na kufanya mikutano ya wananchi pamoja na kutoa matangazo kwa njia mbalimbali, kutoa nyaraka za umilikishaji na madeni na kwa wale ambao walikaidi kulipa madeni walifikishwa kwenye mabaraza ya ardhi kwa hatua zaidi.
Dkt.Mabula kabla ya kufanya kikao hicho alishiriki katika zoezi la mradi wa upimaji mipaka ya vijiji na makazi katika Kijiji cha Mnang'ana wilayani Ikungi ambao unatekelezwa kwa pamoja na mashirika ya UN WOMEN, UNFPA na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ufadhili wa KOICA.